Miaka 17 ya soka la ushindani, sasa imetosha na nahodha wa Simba SC, Musa Hassan Mgosi amecheza game yake ya mwisho kama mchezaji wa timu hiyo wakati Simba SC ikicheza na URA ya Uganda siku ya Jumapili August 14 katika game ya kimataifa ya kirafiki.
SIMBA 2-2 SC Villa, 2005 Tusker Cup
Ilikuwa ni mechi ya kwanza kwa Mgosi kufanya mambo makubwa. Matokeo yakiwa Simba 0-2 Villa na huku mechi hiyo ya nusu fainali ya michuano ya Tusker ikielekea mwishoni, kocha, Mzambia, Patrick Phiri alimnyanyua Mgosi katika benchi na mshambulizi huyo akafunga moja ya magoli bora katika uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Mgosi alifunga mara mbili mbele ya Andy Mwesiga na kusawazisha magoli yote hayo. Simba ikaenda kushinda katika changamoto ya mikwaju ya penati na kutinga fainali kisha kuichapa Yanga SC 2-0 na kutwaa ubingwa. Lilikuwa ni taji lake la pili kushinda.
Awali, Mgosi alishinda taji la FA Cup ‘Kombe la Nyerere’ akiwa na kikosi cha JKT Ruvu ya Pwani.
Wiki mbili baadaye, Mgosi akashinda taji lake la tatu na la pili akiwa mchezaji wa Simba katika michuano ya Tusker Cup 2005 nchini Kenya. Katika michuano hiyo, Simba ilicheza na timu za Asante Kotoko ya Ghana na Super Sports United ya Afrika Kusini.
VPL 2007
Wakati Shirikisho la soka Tanzania ‘TFF’ lilipokuwa likibadili mfumo wa uendeshaji/uchezaji wa ligi kuu-kutoka- Februari hadi Oktoba na kuwa Agosti hadi Mei, ligi kuu Ndogo ikachezwa ili kupata wawakilishi wa Tanzania Bara katika michuano ya CAF 2008, Ligi kuu ya mpito ikachezwa mwaka 2007 ‘Ligi kuu ndogo’ na Simba ikashinda taji hilo kwa kuifunga Yanga katika mchezo wa fainali.
Mgosi alikuwa ni sehemu ya wachezaji muhimu waliofanikisha taji hilo. Alishinda VPL kwa mara yake ya kwanza huku likiwa ni taji lake la nne kushinda.
2008
Mgosi alishinda taji lake la tano, safari hii ikiwa ni lile la michuano ya Kombe la Taifa ‘Taifa Cup’ akiwa na mkoa wa kisoka, Ilala. Pia alikuwa mfungaji bora wa michuano hiyo.
TIMU YA AFRIKA 2009
Wakati, Marcio Maximo alipoiongoza Taifa Stars kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika 2009 kwa wachezaji wa ligi za ndani (CHAN,) Mgosi alikuwa ni kati ya wachezaji waliokuwapo kikosini.
Akiwa na nidhamu ya hali juu mshambulizi huyo mwenye kasi, nguvu, ufundi na uwezo wa hali ya juu katika umiliki wa mpira alicheza game zote tatu za Stars vs waliokuwa wenyeji wa michuano hiyo ya kwanza Ivory Coast, Senegal na Zambia.
Na licha ya Stars kushindwa kufuzu kwa nusu fainali, Shirikisho la soka Afrika-CAF likamteua katika timu ya michuano hiyo ya kwanza. Yalikuwa ni mafanikio mengine makubwa kwa mchezaji huyo.
2009/10
Ni msimu wa mafanikio zaidi kwa klabu ya Simba. Ilishinda taji la VPL pasipo kupoteza mechi yoyote kati ya 22. Mgosi alikuwa ndiye kinara wa mafanikio hayo ya klabu. Alishinda VPL kwa mara ya pili, huku likiwa ni taji lake la sita kushinda.
Yeye binafsi akaingia katika orodha ya wafungaji bora wa ligi kuu. Alifunga jumla ya magoli 14. Ilikuwa ni tuzo yake ya pili ya ufungaji bora.
2011-2016
Baada ya Simba kupoteza kizembe nafasi ya kutetea taji la ligi kuu siku ya mwisho ya msimu, Mgosi hakupewa mkataba mpya huku ‘sababu za kufikirika’ zikichangia. Aliachwa huru baada ya Yanga kushinda taji kwa tofauti ya goli moja.
Eti, ilitajwa sabubu ya Simba. Alinyooshewa vidole vingi hadi na wanachama/mashabiki wa timu hiyo, kwa madai ya kuhujumiwa na baadhi ya wachezaji wao muhimu. Mgosi akaenda DR Congo kucheza soka la kulipwa kwa mwaka mmoja katika timu ya DC Motema Pembe.
Msimu wa 2012/13 alijiunga kwa mara ya pili na JKT Ruvu katika dirisha dogo. Akarejea Mtibwa Sugar kwa mara ya pili katikati ya mwaka 2013. Alidumu hapo kwa misimu miwili na kurejea Simba katikati ya mwaka 2015.
Msimu wa 2015/16 ni wazi ulikuwa wa mwisho kwa mchezaji huyo alifanikiwa kufunga goli moja tu. Ameagwa kwa heshima leo (Jumapili).
Upande wangu nitaendelea kumkumbuka Mgosi kwa mambo mengi mazuri aliyofanya uwanjani. Alitamba hadi katika mapambano makubwa huku baadhi ya magoli yake yakibaki katika kumbukumbu zangu nzuri.
Niseme tu, ‘ Asante Musa Hassan Mg osi kwa kila ulichofanya katika soka.’ Siku zote utabaki ‘Romario wa Tanzania.’ Asante kwa uamuzi wa heshima, kila kitu kizuri kina maisha ya milele. Thamani ya Kitu Kizuri Ni Shida Kushuka Chini Kwa Sababu ya Ubora Wake.
Si hasara kutunza kitu kizuri maana ni pambo katika dunia hii. Uzuri wa kitu ni fahari kubwa katika dunia, tena huleta furaha ambayo aina mwisho kwa watu siku zote. Hali ya uzuri wake haiwezi kupotea bure na thamani yake huwa ya namna moja tu.
Kitu kizuri hakitoki nje kikajitembeza kwa watu, lakini watu wana desturi ya kwenda kukitazama, hata kama kina hali ya namna gani.
Kitu kama hicho hutakiwa na watu wengi, watu hukipa sifa kubwa kitu hicho. kila kitu kizuri kina maisha ya milele. Asante Musa Hassan Mg osi, wewe ni kati ya wale mastraika wafungaji wazuri waliopita.
No comments:
Post a Comment