Magazeti 473 Yafutiwa Usajili
SERIKALI imefuta usajili wa magazeti 473 kutokana na kutochapishwa kwa muda wa miaka mitatu mfululizo.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo, Nape Nnauye alisema magazeti hayo yamefutwa kupitia
tangazo lake lililochapishwa katika Gazeti la Serikali lenye namba 195
la Juni 10, mwaka huu.
Aliyataja
baadhi ya magazeti yaliyofutiwa ni Alasiri, Dar Leo, Femina Magazine,
Sauti ya Wakulima (KCU 1990) Ltd, Utamu, Raha, Starehe, Muongozo,
Motomoto, Daily Times, Financial Times, Sauti ya Siti, Wakati, Hali
Halisi na Mkombozi. Pamoja na magazeti hayo, pia yapo magazeti
yaliyokuwa yanatolewa katika mikoa maalumu kama vile Mbeya Leo,
Kilimanjaro Leo, Arusha Leo, Kigoma Yetu, Karatu Yetu, Tanga Yetu, Sauti
ya Jimbo Kuu Mwanza.
Waziri
Nape alisema kutokana na kufutwa kwa viapo vya usajili wa magazeti
hayo, mtu yeyote atakayechapisha au kusambaza magazeti hayo kwa njia ya
nakala ngumu au kielektroniki atakuwa anakiuka sheria ya magazeti hivyo
atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
“Iwapo
kuna mmiliki wa gazeti ambaye angependa kuendelea na biashara hii baada
ya kufungiwa, milango ipo wazi kwa ajili ya kuwasilisha maombi mapya ya
usajili kwa kufuata taratibu zilizopo, ni imani yangu kuwa kwa wale
wenye nia njema wameyaelewa maelezo haya,” alisema Nape.
Pia
amewataka wamiliki wa magazeti hayo yaliyofutiwa viapo wahakikishe
kwamba hawavunji sheria kwa kuanza biashara bila kufuata taratibu za
usajili upya na endapo watakiuka maelezo hayo hatua kali za kisheria
zitachukuliwa dhidi yao.
No comments:
Post a Comment