WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene (pichani), ameagiza Kaimu Ofisa Biashara wa Manispaa ya Ilala, Dennis Mrema asimamishwe kazi kutokana na madai ya kusababisha upotevu wa mapato ya serikali.
Alimwagiza Mkurugenzi wa Manispaa hiyo amsimamishe kazi Mrema kuanzia jana akieleza kuwa urasimu wa kukusudia, mazingira ya rushwa na uzembe katika utoaji leseni za biashara vimesababisha upotevu wa mapato ya serikali.
Uamuzi huo unaelezwa kutokana na malamiko mengi ya wafanyabiashara dhidi ya mtendaji huyo kuwa amekuwa akikiuka sheria, kanuni na taratibu za kutoa leseni, urasimu na rushwa. Ilielezwa kuwa, uchunguzi wa awali katika Halmashauri ya Manispaa ulibaini kukiukwa kwa sheria, kanuni na taratibu hizo.
Pia, ilibainika kutolewa leseni za biashara zaidi ya 843 bila kuwa na vyeti vya uthibitisho wa walipa kodi (Tax Clearance Certificates), hivyo kuikosesha serikali kodi ya mapato. Madai mengine yaliotajwa ni kuwepo fomu za wafanyabiashara 336 zilizokaa kwa muda mrefu bila sababu za msingi, pamoja na kukiuka mwongozo wa mkataba wa huduma kwa wateja ambao unamtaka Ofisa Biashara kutoa leseni ndani ya siku mbili hadi tatu, baada ya muombaji kuwasilisha maombi yake.
No comments:
Post a Comment