MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), imesema inaendelea na mchakato wa kupokea maoni ya wadau mbalimbali kuhusu nauli zitakazotumika kwa ajili ya usafiri wa mabasi yaendayo kasi, na itahakikisha inatoa nauli zinazoendana na halisi halisi.
Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Meneja Mawasiliano wa Sumatra, David Mziray alisema wanafanyia kazi taarifa ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ya kukataa mapendekezo ya nauli yaliyotolewa na kampuni ya UDA Rapid Transit (UDA-RT) .
“Kama alivyosema Waziri Mkuu kuwa mapendekezo ya nauli hizi ni ya gharama kubwa na hata tulivyokutana na wadau kujadili mapendekezo haya wengi waliyapinga sasa sisi tunaendelea kukusanya maoni hadi Januari 13, baada ya hapo tutatoa uamuzi wa nauli ambazo hazitakandamiza upande wowote,” alisema Mziray.
Alisema mamlaka hiyo haitarejea tena mchakato wa kupokea mapendekezo mapya ya nauli kutoka kampuni ya UDA-RT bali itaendelea na utaratibu wa kukusanya maoni kutoka kwa wadau ambapo itatoa uamuzi kulingana na maoni hayo ya wadau.
Kampuni ya UDA-RT hivi karibuni ilitoa mapendekezo ya nauli inayotarajia zitumike katika mradi wa usafiri wa mabasi yaendayo haraka (DART) ambazo ni safari kwenye njia kuu kuwa Sh 1,200 na safari katika njia kuu na pembeni kuwa Sh 1400 na wanafunzi nusu ya nauli hizo.
Waziri Mkuu aliagiza taasisi zinazohusika; Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ya Ujenzi na ya Uchukuzi, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) pamoja na kampuni ya UDA-RT kukutana haraka kujadili viwango vipya vya nauli vinavyoendana na hali halisi ya maisha ya wananchi.
Licha ya Waziri Mkuu kupinga nauli hizo, wadau wengine hususan Baraza la Walaji la Sumatra (Sumatra CCC), walihoji sababu za mabasi hayo yanayobeba watu wengi kwa safari moja na yanayotumia barabara zisizo na foleni, kutoza nauli kubwa.
No comments:
Post a Comment