Wednesday, 6 January 2016
simba yashinda bao 1-0 dhidi ya URA Hajibu ndiye mfalme wa jana
SIMBA SC imebisha hodi Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi 2016, kufuatia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya URA ya Uganda katika mchezo wa Kundi A usiku huu Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Shujaa wa Simba SC, alikuwa Ibrahim Hajib Migomba aliyefunga bao hilo pekee dakika ya
37 kwa shuti lake la umbali wa mita 20, baada ya kupokea pasi ya beki Mrundi, Emery Nimubona.
Simba SC inapanda kileleni mwa Kundi A baada ya kufikisha pointi nne, kutokana na mechi mbili, ikifuatiwa na URA yenye pointi tatu sawa na JKU, wakati Jamhuri wanashika mkia kwa pointi yao moja.
Simba SC, mabingwa watetezi wa Kombe hilo, ilistahili ushindi katika mchezo wa leo, kutokana na kucheza kwa umakini na nidhamu ya hali ya juu, kiasi cha kuwadhibiti kabisa URA.
Na ingeweza kutoka na ushindi mnene zaidi iwapo, washambuliaji wake wangetumia nafasi zaidi walizopata.
Dakika ya 51, Danny Lyanga alimtoka vizuri Jimmy Kulaba, lakini shuti lake likatoka nje, wakati dakika ya 70, kipa wa URA, Brian Bwette alifanya kazi ya ziada kupangua mpira wa kichwa wa Mganda mwenzake, Hamisi Kizza aliyemalizia pasi ya Mwinyi Kazimoto
Michuano hiyo itaendelea kesho kwa mechi za Kundi B kuhitimishwa, Azam FC wakimenyana na Mafunzo, wakati Yanga SC watamenyana na Mtibwa Sugar usiku.
Simba SC itamaliza na JKU keshokutwa, wakati URA itamaliza na Jamhuri.
Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Peter Manyika, Emery Nimubona, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’/Brian Majwega dk64, Abdi Banda, Juuko Murushid, Justice Majabvi, Mwinyi Kazimoto, Said Ndemla, Ibrahim Hajib/Awadh Juma dk83, Hamisi Kizza/Mussa Mgosi dk83 na Danny Lyanga.
URA; Brian Bwette, Simeon Massa/Sharifin Kagimu dk47, Allan Munaaba, Jimmy Kulaba, Sam Senkoom, Oscar Agaba, Julius Ntambi, Said Kyeyune, Derrick Tekwo/Ronald Kigongo dk47, Villa Oromuchani na Elkanah Nkagwa/Peter Iwassa dk75.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment