WAZIRI wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba amemsimamisha Kazi Mkurugenzi Mkuu wa Ranchi za Taifa pamoja na Wakurugenzi wa Bodi ya Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kutokana na madai ya ubadhirifu wa fedha. Amechukua hatua hiyo baada ya kubaini ubadhirifu wa Sh bilioni 5.7 zilizotolewa kwa ajili ya ujenzi wa machinjio ya kisasa ya Ruvu ambayo yalizinduliwa na Jakaya Kikwete (Rais mstaafu) mwaka 2010 .
Nchemba alichukua hatua hiyo baada ya kufanya ziara ya siku moja kwenye ranchi ya Taifa ya Ruvu kukagua ujenzi wa majengo ya machinjio ya kisasa ulioanza mwaka 2010 ambao hadi sasa haujamalizika.
Ilielezwa kuwa gharama za ujenzi wa machinjio hayo ya kisasa ni Sh bilioni 10.7 na serikali ilishatoa nusu ya gharama hizo lakini kwa uzembe au makusudi Mkurugenzi wa Ranchi za Taifa hajasimamia jengo hadi kuisha.
Alisema jengo hilo mpaka lilipofikia, limetumia Sh bilioni 2.7 hivyo Sh bilioni tatu, haijulikani zilipo huku Bodi ya Narco ikipendekeza kusitishwa kwa ujenzi wa jengo hilo na kujenga lingine kwa gharama nyingine.
Alisema Waziri alikataa na kuamua kufukuza wakurugenzi wote wa Bodi ya Narco. Aliivunja rasmi bodi nzima na kumsimamisha kazi Mkurugenzi wa Ranchi za Taifa kutokana na kushindwa kusimamia mali za umma na kusababisha hasara hiyo.
Alisema amekutana na ubadhirifu wa Sh bilioni 5.7 ambazo zilitolewa kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo. Alisema fedha hizo zilizokuwa zimelengwa kuwezesha ujenzi wa machinjio hayo ya kisasa hazijafanya kazi kama ilivyokusudiwa.
Alisema amekuta mradi huo umetelekezwa tangu mwaka 2010 bila kuendelezwa huku wakidai mradi huo ulitelekezwa baada ya kutofautiana kwa mkandarasi na Bodi ya Narco.
“Mbali na kushindwa, bodi hiyo imeutelekeza mradi huo na hivi sasa inapendekeza kujengwa kwa mradi mwingine kama huo ndani ya eneo hilo hilo la ranchi ya Ruvu,” ilielezwa.
Mwigulu alisitisha utumishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Ranchi za Taifa, kwa kushindwa kuchukua hatua za kusimamia ujenzi wa mradi huo hadi kukamilika kwake. Machi mwaka jana, ilielezwa kuwapo mpango wa NARCO kuanza ujenzi wa machinjio ya kisasa huko Ruvu mkoa wa Pwani yenye uwezo wa kuchinja ng’ombe 800 kwa siku, wakati tayari kulikuwa na mradi mwingine uliotakiwa kuendelezwa.
Waziri Mwigulu aliagiza vyombo vya sheria kuhakikisha wahusika wote walioshiriki ama kwa makusudi au kwa njia yoyote kuhujumu mradi huo usifanikiwe wakiwemo washauri elekezi, wajenzi kuchukuliwa hatua haraka iwezekanavyo.
Huku akiagiza wataalamu wa wizara kuhakikisha ndani ya siku saba wanampelekea ripoti ya thamani ya jengo lililokwisha kujengwa na fedha zinazotakiwa kumalizia ujenzi wa jengo hilo ili fedha itengwe na mradi kukamilika.
No comments:
Post a Comment