“Kesi zinazopokelewa katika maabara yetu zinazohusu sampuli ya vinasaba kwa mwaka zinaonesha kuwa asilimia 49 kati ya asilimia 100 ya matokeo hayo, huonyesha mzazi mmoja ambaye ni baba kuwa si mzazi halali wa mtoto huyo,” alifafanua Profesa Manyele na kuongeza: “Vinasaba ni utambulisho wa kipekee wa kila kiumbe ambao unabeba taarifa muhimu na inayorithisha tabia au umbile fulani la mhusika.
Vinasaba ni kama vile kitabu cha kumbukumbu kinachohusu maisha binafsi.” Profesa Manyele aliongeza kuwa mikoa ya kanda ya Ziwa, Arusha, Dar es Salaam na Mbeya, ndio inayoongoza kwa matokeo ya uchunguzi huo wa makosa ya vinasaba nchini.
Akizungumza kuhusu lengo la mkutano huo, Profesa Manyele alisema ni kuimarisha uhusiano uliopo kati ya wadau wa kemikali na wadau wa afya ya mazingira kutoka katika Halmashauri nchini pamoja na Ofisi ya Mazingira.
Aidha, Profesa Manyele alibainisha baadhi ya majukumu yanayofanywa na Wakala wa Mkemia Mkuu wa Serikali kuwa ni kufanya uchunguzi ili kuhakiki ubora na usalama wa vyakula, dawa, maji, maji machafu, bidhaa za viwanda na mashambani, sampuli za mazingira na sampuli zinazohusiana na makosa ya jinai.
“Matokeo ya uchunguzi wa makosa ya jinai na vinasaba huviwezesha vyombo husika kufikia maamuzi stahili na kusaidia kutendeka kwa haki katika tuhuma za kesi za jinai ikiwemo ulevi, mauaji, ubakaji, wizi wa watoto, uhalali wa mtoto kwa mzazi, kwa kupitia vyombo husika,” alifafanua.
No comments:
Post a Comment