RAIS John Magufuli amevunja Kamisheni ya Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) na kuwasimamisha kazi watendaji wakuu wa tume hiyo baada ya kubainika kudahili wanafunzi wasio na sifa na kuwapa mikopo.
Pia
serikali imetangaza kufanyika kwa udahili upya Vyuo Vikuu vyote nchi
nzima ili kuwaondoa vyuoni wanafunzi wote wasio na sifa sambamba na
kutangaza vita kali kwa wanafunzi hewa wanaopata mikopo ya elimu ya juu.
Hayo
yamebainishwa leo na Prof. Joyce Ndalichako Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia alipozungumza na waandishi wa habali juu ya kuvunjwa kwa
Kamishina ya TCU.
Amesema, kwa idhini aliyopewa na rais anawasimamisha kazi mara moja watendaji hao wa Kamisheni ya Tume ya Vyuo Vikuu.
Prof.
Ndalichako amewataja waliosimamishwa kazi kuwa ni Prof. Yunus Mgaya,
Katibu Mtendaji wa TCU kwa kushindwa kusimamia kazi za TCU akiwa kama
mtendaji mkuu wa taasisi hiyo.
Pia,
Dk. Savius Maronga, Mkurugenzi wa Udhibiti na Ubora kwa kushindwa
kutekeleza wajibu wake wa kusimamia ubora na ithibati ya Vyuo Vikuu.
Amesema
Rose Kiishweko, Mkurugenzi wa Udahili amesimamishwa kwa kushindwa
kusimamia udahili wa wanafunzi na kupelekea kudahiliwa wanafunzi wasio
na sifa, na mwingine aliyesimamishwa ni Kimboka Istambuli ambaye
alikuwa Kaimu Mkurugenzi wa Udahili na Nyaraka.
Mbali
na hilo Prof. Ndalichako amesema, ili shughuli za TCU ziendelee, Prof.
Eliuter Mwageni ameteuliwa kukaimu nafasi ya katibu mtendaji na kabla
ya uteuzi wa kukaimu nahfasi hiyo Prof. Mwageni alikuwa Naibu Makamu
Mkuu (Utawala na Fedha) wa Chuo Kikuu cha Ardhi.
Aidha
ameteuliwa Dk. Kokubelwa Mollel ambaye atakaimu nafasi ya ukurugenzi wa
udahili na nyaraka na kabla ya uteuzi wa kukaimu nafasi hiyo Dk.
Kokubelwa alikuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Amesema kwa muda mrefu kumekuwa na taarifa za wanafunzi wa Chuo Kikuu cha St. Joseph wanaodahiliwa kutokuwa na sifa.
Waziri
amesema, kutokana na hilo serikali imeamua kutoa tamko baada ya ukaguzi
kufanyika katika chuo hicho katika kampasi za Arusha na Songea na
kubaini kuwepo kwa upungufu mkubwa katika utoaji wa elimu isiyokuwa na
kiwango.
Amesema,
walibaini kuwepo kwa wanafunzi 489 ambao wapo katika vyuo hivyo ambao
hawakidhi viwango na hawana sifa za kusoma Chuo Kikuu.
Amesema
kibaya zaidi ni kuwepo kwa wanafunzi ambao ni wa kidato cha nne
waliofaulu Daraja la Nne huku wengine wakiwa na pointi 32 lakini
wakidahiliwa kusomea shahada ya kwanza .
“Mwanafunzi
wa Kidato cha Nne anasoma digrii ya Sayansi, huku mtu huyo akiwa
sekondari kasoma mkondo wa biashara lakini kadahiliwa asomee Sayansi na
analipiwa mkopo na TCU.
“Si
tu hana sifa ya kusoma Chuo Kikuu, hana hata sifa ya kuwa na cheti cha
ualimu kwa maana hiyo mtu wa aina hiyo hafai hata kuwa na cheti cha
ualimu hatuwezi kukubali mtu wa jinsi hiyo akasomee digrii,” amesema.
Prof.
Ndalichako amesema rais amekuwa akihangaika kutafuta fedha kwa ajili ya
mikopo ya elimu ya juu lakini cha kusikitisha kuna wanafunzi waliofaulu
vizuri Kidato cha Sita wanakosa mikopo ila wale waliofeli wanapata
mikopo hiyo.
“Divisheni four pointi 34 yuko Chuo Kikuu hata ualimu simkubali mtu wa namna hiyo,” amesema.
Amesema,
baada ya serikali kufunga chuo hicho wanafunzi hao walihamishiwa vyuo
vingine lakini hata huko walikopelekwa uwezo wao umeonekana kuwa ni
mdogo hali iliyolazimu kuwarudisha madarasa ya nyuma.
‘Wanafunzi
waliotoka St. Joseph na kupelekwa Chuo Kikuu cha Dodoma uwezo wao
umeonekana kuwa ni mdogo, ambapo wanafunzi wa mwaka wa pili na wa kwanza
wamerudishwa nyuma muhula moja huku wale wa mwaka wa tatu wamerudishwa
nyuma mwaka moja” amesema.
Amesema,
wale wa St. Joseph Tawi la Songea waliopelekwa Chuo Kikuu cha Kilimo
Morogoro (SUA) waliokuwa wakisoma mwaka wa nne wamerudishwa mwaka wa
tatu na wametengewa vipindi vya ziada ili kurekebisha upungufu huo, na
hata wale waliopelekwa vyuo vingine vya Ruaha, Mkwawa wameonekana kuwa
na upungufu pia.
“Kibaya
zaidi hao wanafunzi walikuwa wanapata mikopo, Division four anapata
mkopo haki iko wapi, tulipoona jambo hili si sawa, tulichukua hatua
tukaieleza bodi ya TCU kusimamisha kazi waliohusika lakini hilo
halikufanyika,” amesema.
Kufuatia
kuwepo kwa matatizo hayo Prof. Ndalichako ametangaza vita kwa vyuo
mbalimbali ambavyo vina watu ambao wanadahili wanafunzi wasio na sifa.
Kuhusu
wanafunzi ambao hawakuwa na sifa lakini walikuwa wakisoma chuo kikuu
hicho amesema licha ya kuwa wamepoteza muda wao mwingi lakini
watalazimika kurejesha mikopo hiyo.
“Wale
wote ambao walipata mikopo bila kuwa na sifa watarejesha mikopo hiyo na
hakuna njia yoyote ya kuwasaidia bali wanatakiwa kuendelea kuangalia ni
jinsi gani ya kujiendeleza,” amesema.
No comments:
Post a Comment