Friday, 1 April 2016

KAPOMBE ATASHINDA TENA TUZO YA MCHEZAJI BORA VPL KWA MARA YA PILI

Shomari Kapombe-Beki Azam FC

MICHEZO kumi kuelekea mwishoni mwa msimu wa ligi kuu Tanzania Bara ( VPL,) mlinzi wa pembeni wa klabu ya Azam FC, Shomari Kapombe anastahili kushinda tuzo yake ya pili ya mchezaji bora wa msimu. Kapombe, 24 alishinda tuzo ya mchezaji bora wa VPL msimu wa 2011/12 wakati alipoisaidia Simba SC kushinda ubingwa.
Msimu wake wa pili katika kikosi cha Azam FC unakwenda vizuri. Mlinzi huyo namba mbili wa timu ya Taifa (Taifa Stars) tayari amefanikiwa kufunga magoli 8 katika VPL wakati timu yake ikiwa imekwisha cheza michezo 20.
Alhamis hii mchezaji huyo zao la ‘Moro Kids’ alifanikiwa kufunga magoli mawili katika mchezo wa hatua ya robo fainali ya michuano ya kombe la FA. Magoli hayo mawili aliyofunga katika ushindi wa Azam FC 3-1 Tanzania Prisons yamemfanya Kapombe kufikisha jumla ya magoli kumi msimu huu na hivyo kuwa mlinzi pekee aliyefunga magoli mengi msimu huu.
Juma Abdul alifunga magoli nane akicheza kama mlinzi katika timu ya Toto Africans ya Mwanza msimu wa 2010/11, Stefano Mwasyika pia amewahi kumaliza msimu wa 2007/08 kama mlinzi aliyefunga magoli mengi katika VPL.
Mwasyika mlinzi wa kushoto wa zamani wa Yanga SC na Taifa Stars alitamba kwa magoli yake ya mikwaju ya penalti na mipira ya faulo. Wakati, Mwasyika na Juma Abdul walitumia mipira mingi iliyokufa, Kapombe yeye amekuwa akifunga kwa kuwa amekuwa akipanda sana kwenda mbele wakati timu yake ikishambulia.
Licha ya mfumo wa kocha Stewart Hall kumruhusu kwenda mbele, kikawaida jitihada zake binafsi, uwezo na utulivu umemfanya Kapombe kufunga magoli ya kutosha hadi sasa. Azam hushambulia kupitia pembeni ya uwanja na sehemu hiyo imechangia kuwafanya Kapombe na kinara wa ufungaji katika timu hiyo Mu-ivory Coast, Kipre Tchetche kupata nafasi nyingi za kufunga.
Kitu kinachomsaidia sana Kapombe ni uwezo wake wa kuanzisha mashambulizi akitokea katika beki 2, si hivyo tu amekuwa akifuatilia ‘move’ zote za mashambulizi na pindi anapokutana na mpira katika eneo la hatari la timu pinzani hujibadilisha kutoka ‘tabia za mlinzi na kujivisha tabia za mshambuliaji’.
Kwa sasa Kapombe anathibitisha namna alivyo mlinzi bora wa kulia nchini. Anacheza kwa nguvu, kasi na akili huku akiwa na uwezo mkubwa wa kumiliki mpira.
Wakati Simba wanatamba na Hassan Kessy-kijana mwingine zao la Moro Kids, Yanga wakitamba na Juma Abdul kijana mwingine kutoka Kingalu Kids-timu ya vijana iliyokuja kuungana na Moro Kids na kutengeneza Moro Youth Soccer Academy, Shomari Kapombe kwa sasa ana kaa juu ya vijana hao wengine na kujiweka katika daraja la peke yake kama mlinzi bora, bora zaidi namba mbili.
Ndiyo, VPL ina washambuliaji wakali msimu huu kama Hamisi Kizza, Amis Tambwe, Donald Ngoma, Kipre Tchetche, Jeremiah Juma na wengineo waliofunga magoli mengi zaidi ya Kapombe lakini itanishangaza sana kama tuzo ya mchezaji bora wa msimu haitakwenda kwa Kapombe.
Amejibidiisha sana na magoli yake yameibeba klabu yake kwa kiasi kikubwa hadi sasa. Shomari Kapombe anavyosaka tuzo yake ya pili ya mchezaji bora wa VPL mbele ya mastaa wa kigeni inapendeza sana. Kapombe atashinda tena tuzo ya mchezaji bora VPL kwa mara ya pili.

No comments:

Post a Comment