Watu
wawili wameuawa Jijini Mwanza kwa kupigwa risasi na Majambazi, huku
Wengine saba wakijeruhiwa katika tukio la uvamizi wa duka lililokuwa
likitoa huduma mbalimbali za kifedha.
Kamanda
wa Polisi Mkoani Mwanza, Justus Kamugisha, amesema kuwa tukio hilo
lilitokea jana majira ya saa mbili usiku katika eneo la Bugarika Sokoni,
baada ya watu watatu wanaosadikika kuwa ni majambazi waliokuwa na
bunduki aina ya SMG kuvamia katika duka la mfanyabiashara na mkazi wa
eneo hilo aitwae Daniel Marwa (30).
Kamanda
Kamugisha amewataja waliouawa kuwa ni Julius Wankaba (30) ambae ni
dereva bodaboda, pamoja na mfanyabiashara mmoja mwenye duka katika eneo
hilo aliefahamika kwa jina la Mama Yuni (35).
Amewataja
waliojeruhiwa kuwa ni Magesa Mungari (38), Simioni Charles (26) ambao
wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa Bugando huku wengine wakiwa ni Mwita
Ryoba (30), Frank Willium (19), Saumu Said (20), Masumbuko Kanduru (38)
pamoja na Emmanuel Francis ambao wanapata matibabu katika Hospital ya
Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekour Toure.
Baadhi
ya Mashuhuda wa tukio hilo, akiwemo mmiliki wa duka lililovamiwa,
wanasema majambazi hao walipofika eneo la tukio walianza kufyatua risasi
ovyo ili kuwatawanya wananchi waliokuwa wamekusanyika katika eneo hilo
wakiangalia taarifa ya habari na wengine wakinywa kahawa, na hivyo
kusababisha wananchi kutawanyika jambo lililosababisha vifo na majeruhi
hao.
Katika
tukio hilo, Majambazi hao walifanikiwa kupora fedha taslimu kiasi cha
Shilingi Milioni Mbili, Vocha za simu za mitandao mbalimbali
zinazokadiliwa kuwa za shilingi Laki Nane pamoja na simu sita za wateja.
Kamanda
Kamugisha amesema Jeshi la polisi Mkoani Mwanza limeanzisha msako mkali
ili kuwakamata waliohusika na tukio hilo, huku likiahidi zawadi ya
fedha kiasi cha shilingi Milioni Moja kwa yeyote atakaesaidia kufanikiwa
kukamatwa kwa watuhumiwa hao.
Wakati
huo huo, Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza linaendelea kumsaka mtu
aliehusika na wizi wa mtoto mwenye umri wa siku moja katika Hospitali ya
Wilaya ya Magu, ambapo tukio hilo limetokea Machi 23 mwaka huu, majira
ya saa nane mchana baada ya mtu mmoja asiefahamika mwenye jinsia ya
kike, kufika katika wodi ya wazazi na kumuiba mtoto huyo wakati mama
yake amelala.
Aidha
katika katika kusherehekea Sikukuu ya Pasaka, Jeshi hilo limepiga
marufuku watoto kwenda kuogelea katika fukweni (Beach) pamoja na uwepo
wa disko toto Jijini Mwanza.
No comments:
Post a Comment