Kikosi
cha timu ya Taifa ya Tanzania “Taifa Stars” inayodhaminiwa na bia ya
Kilimanjaro Premium Lager kimekamilika baada ya kundi la pili lenye
wachezaji nane kuwasili leo mchana nchini Chad tayari kwa mchezo wa
kesho dhidi ya wenyeji kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa Afrika
(AFCON) mwaka 2017.
Kundi hilo la pili limewasili
majira ya saa sita mchana (saa za Chad) likiongozwa na mkuu wa msafara
ambaye pia ni Rais za ZFA, Ravia Idarus na kupokelewa na viongozi
waliopo jijini N’Djamena.
Mara baada ya kuwasili D’jamena
wachezaji walipata nafasi ya kupumzika hotelini kabla ya kuelekea
mazoezini kufanya mazoezi ya pamoja kwa wachezaji wote, yakiwa ni
mazoezi ya mwisho kabla ya mchezo wa kesho.
Kocha Mkuu wa Taifa Stars Charles
Mkwasa amekiongoza kikosi chake chenye jumla ya wachezaji 20 kufanya
mazoezi mepesi saa 9 mchana katika uwanja wa Idriss Mahamat Ouya uliopo
jijini N’Djamena.
Katika mazoezi ya leo wachezaji wa
Taifa Stars walionekana kuwa na umakini mkubwa katika kusikiliza
maelekezo ya kocha Mkwasa, huku morali ya wachezaji ikiwa juu kuelekea
kusaka pointi 3 muhimu katika mchezo huo.
Wachezaji waliopo Chad ni
magolikipa Aishi Manula na Ally Mustafa, walinzi Shomari Kapombe, Juma
Abdul, Haji Mwinyi, Mohamed Hussein, David Mwantika, Erasto Nyoni na
Kelvin Yondani.
Viungo ni Himid Mao, Jonas Mkude,
Mwinyi Kazmito, Mohamed Ibrahim, Farid Musa, Deus Kaseke na Shiza
Kichuya, huku washambuliaji wakiwa ni John Bocco, Ibrahim Ajibu, Thomas
Ulimwengu na nahodha Mbwana Samatta.
Mechi kati ya Chad dhidi ya
Tanzania inatarajiwa kuchezwa kesho Jumatano saa 9:30 (saa 11:30 kwa saa
za Tanzania) katika uwanja wa Idriss Mahamat Ouya jijini N’Djamena, na
utarushwa moja moja na kituo cha luninga cha Taifa cha Chad (Tele Chad).
No comments:
Post a Comment