Monday, 7 March 2016

Mwanafunzi Atoroka Bwenini Usiku, Abakwa na Kisha Kunyongwa


Mwanafunzi  wa bweni wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya kata ya Mnero, tarafa ya Ruponda, wilaya ya Nachingwea, mkoani Lindi, Agnes Jeremiah (18) ameuwawa kwa kunyongwa na watu wasiofahamika usiku kisha mwili wake kutupwa kichakani.

Habari za uhakika kutoka wilayani humo na ambazo zimethibitishwa na Jeshi la Polisi zinaeleza mwanafunzi huyo alinyongwa Februari 27, mwaka huu saa 4:30 usiku.

Mashuhuda wamesema kuwa Agnes alikuwa na tabia kutoroka bwenini nyakati za usiku na kwenda nje ya shule.

“Taarifa ambazo tunazisikia huyu marehemu alikuwa akitoroka bwenini usiku na kwenda anakokufahamu mwenyewe kabla ya kurejea alfajiri,” alisema mmoja wa watoa  ambaye hakupenda jina lake litajwe

Kamanda wa Polisi mkoani Lindi, Renatha Mzinga amekiri kutokea kifo cha mwanafunzi huyo, na kueleza uchunguzi walioufanya umebaini alikuwa ni tabia ya kutoroka bwenini nyakati za usiku na kwenda kwa mpenzi wake wa kiume.

“Ni kweli taarifa ya kifo cha huyo mwanafunzi Agnes Jeremiah ambaye ni mkazi wa kijiji cha Mandawa, akiwa bwenini huko Mnero Sekondari alitoroka usiku kwenda kwa mwanaume,” alisema Mzinga.

Mzinga alisema uchunguzi unaonyesha mwanafunzi huyo alipofika eneo la kichaka kilichopo karibu na kanisa la Roma, alibakwa na wanaume kisha kunyongwa shingo na mwili wake kutelekezwa papo hapo.

Akasema katika kufuatilia tukio hilo, wanamshikilia mkazi wa kijiji cha Mnero Ngongo, Abdallah Ismaili (19) ambaye ni dereva wa bodaboda kwa mahojiano zaidi.

”Inasemekana huyu dereva wa bodaboda ndiye aliyekuwa akienda Shuleni hapo kumchukuwa na kumpeleka kwa mwanaume wake ambaye kwa sasa ametoweka kijijini hapo,” alisema Mzinga.

Hata hivyo, kamanda huyo wa Polisi Lindi hakuwa tayari kutaja jina la mwanaume anayedaiwa kuwa na mahusiano na mwanafunzi huyo, kwa maelezo kwamba anaweza kuvuruga upelelezi.

“Tunaendelea kumsaka huyu mwanaume wake aliyekuwa akipelekwa mwanafunzi huyu, hivyo iwapo tutamtaja jina tunaweza kuharibu upelelezi wetu.

No comments:

Post a Comment