Shirikisho la Soka la Chad, limetangaza kuiondoa timu yake ya taifa
katika mechi za kuwania kufuzu Fainali za Afrika zitakazofanyika nchini
Gabon mwakani.
Tanzania na Chad zilikuwa zicheze leo, mechi ya
marudiano ya kuwania kufuzu fainali hizo. Katika mchezo wa kwanza, Stars
iliifunga Chad bao 1-0, mchezo uliofanyika kwenye mji wa N’Djamena.
Mtandao
wa Twitter wa Shirikisho la Soka Afrika, CAF ulithibitisha jana kupokea
taarifa ya Chad na tayari limetangaza adhabu ya kuisimamisha nchi hiyo.
“Shirikisho la Soka la Chad limeondolewa kushiriki mashindano
yajayo ya Afcon na linatakiwa kulipa faini ya Dola 20,000,” ilisema
taarifa hiyo ya CAF kwa kifupi.
Kujitoa kwa Chad kumevuruga
msimamo wa Kundi G la michuano hiyo kwani kwa mujibu wa Kanuni za
Mashindano ya CAF, Ibara ya 58 inasema: “Ikiwa timu itajitoa kwenye
mashindano hatua za awa li za makundi, matokeo yote yatafutwa (pointi,
mabao ya kufunga na kufungwa).
Ibara ya 59 ya kanuni hizo za mashindano inasema Kamati ya Maandalizi itatoa adhabu kali kulingana na uzito wa timu kujitoa.
Kwa hatua hiyo, Misri iliyoshinda mabao 5-1, Nigeria 2-0 na Tanzania 1-0 zitakuwa zimepoteza matokeo hayo.
Kwa mujibu wa kanuni, Misri sasa itakuwa na pointi nne ikifuatiwa na Nigeria pointi mbili na Tanzania itabakia na pointi moja.
Michezo
itakayobakia ni ya Misri kuifunga Tanzania 3-0 na sare ya 1-1 dhidi ya
Nigeria wakati Taifa Stars inabakiwa na pointi moja ya suluhu na
Nigeria. Nigeria itabakia na pointi mbili za Tanzania na Misri kabla ya
mchezo wao wa kesho kwenye mji wa Alexandria.
Mratibu wa timu ya
Taifa, Msafiri Ahmed Mgoyi alikiri kuziona taarifa za Chad kutocheza
mchezo na kusema: “Tumezipata taarifa hizo lakini bado tunaendelea
kujiandaa kama kawaida mpaka pale tutakapopata taarifa rasmi kutoka TFF
ambao wanapokea maelekezo kutoka Caf.”
Rais wa Shirikisho la
Soka Tanzania, TFF, Jamal Malinzi alisema jana kupitia ukurasa wake wa
Twitter kuwa iwapo Chad itashindwa kucheza mchezo, uamuzi wa mwisho
utatolewa na chombo husika kinachosimamia mashindano hayo.
“Hadi
sasa timu ya Chad haijatua nchini kwa ajili ya mechi ya kesho. TFF
itatoa taarifa kamili leo usiku (jana) baada ya kikao cha maandalizi ya
mchezo. Kwa mujibu wa kanuni za CAF Kamati ya Maandalizi ya mashindano
ya Caf ndiyo inatoa uamuzi,” alisema Malinzi.
Kocha Msaidizi wa
Taifa Stars, Hemed Morocco alisema jana kuwa benchi la ufundi na
wachezaji kama ilivyo kwa watu wengine nao wamezipata taarifa hizo
ingawa haziwezi kuathiri saikolojia yao kwa namna yoyote ile.
“Sisi
kwa upande wetu tunafahamu mechi ipo kama kawaida kwani hatujapewa
taarifa yoyote kutoka kwa TFF, hivyo kama ni kweli au la haiwezi
kuvuruga mipango na maandalizi yetu kama timu, ingawa ufafanuzi zaidi
tunausubiri,” alisema Morocco.
Wakati hali hiyo ikitokea,
mashabiki wa soka walikwishaanza kukata tiketi za mchezo kati ya
Sh25,000 ikiwa ni kiingilio cha juu na Sh5,000.
No comments:
Post a Comment