Wednesday, 13 January 2016
SIMBA, STAND ZAPIGWA FAINI!
Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imeipiga faini ya sh. 500,000 (laki tano) klabu ya Stand United baada ya timu yake kupata kadi zaidi ya tano kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom dhidi ya Coastal Union iliyofanyika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga. Katika mechi hiyo iliyochezwa Desemba 26, 2015, timu hiyo ilipata kadi saba kinyume na Kanuni ya 42(11) ya Ligi Kuu.
Wachezaji Fred Mbuna wa Majimaji, na Hamad Kibopile wa Mbeya City watafikishwa kwenye Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kutokana na kufanya vitendo vya utovu wa nidhamu wakati wa mechi kati ya timu zao dhidi ya Azam na Yanga.
Kibopile aliwatolewa waamuzi lugha za kudhalilisha wakati wa mapumziko kwenye mechi dhidi ya Yanga, huku Mbuna akipiga teke chupa ya maji, na maji hayo kuwarukia waandishi wa habari wakati wakiripoti mechi hiyo mjini Songea.
Simba imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na washabiki wake kumrushia mwamuzi msaidizi namba moja chupa za maji na makopo ya bia wakipinga kuashiria mshambuliaji wa Simba kuotea dakika ya 57. Pia walifanya hivyo dakika ya 80 kwenye mechi hiyo dhidi ya Mwadui iliyochezwa Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
Timu ya Toto Africans imepewa onyo kwa kuchelewa uwanjani kwa dakika 23 kwenye mechi yao dhidi ya African Sports iliyofanyika Desemba 27, 2015 katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment