Wednesday, 13 January 2016

Iran yawaachilia huru wanamaji wa Marekani

Iran


Wanajeshi wa Iran wamewaachilia huru mabaharia 10 wa Marekani waliokuwa wamekamatwa na kuzuiliwa kwa kuingia eneo la bahari la Iran, runinga ya taifa imeripoti.
Walikamatwa Jumanne wakiwa kwenye boti mbili, baada ya boti moja kupata hitilafu za kimitambo wakati wa mazoezi, Marekani imesema.
Taarifa iliyosomwa runingani nchini Iran imesema wanamaji hao wameachiliwa na kuruhusiwa kuingia eneo la bahari la kimataifa baada yao kuomba radhi.
Afisa wa Marekani amethibitishia shirika la habari la Reuters kwamba mabaharia hao wameachiliwa huru.
Waliingia maeneo ya Iran bila kukusudia, taarifa kutoka kwa wanajeshi wa Revolutionary Guards iliyonukuliwa katika runinga ya taifa imesema.
Awali, kamanda wa kikosi cha wanamaji cha Revolutionary Guards, Jenerali Ali Fadavi, alikuwa amesema uchunguzi ulikuwa umeonyesha hitilafu katika mitambo ya kuelekeza boti zilichangia.
"Tumethibitisha kwamba kuingia kwa Wamarekani hao maeneo yetu ya bahari hakukuwa uchokozi au kwa kusudi la kupeleleza au masuala husika,” aliambia runinga ya taifa ya Iran.

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani John Kerry alimpigia simu mwenzake wa Iran Javad Zarif muda mfupi baada ya kisa hicho kutokea.
Wawili hao waliunda urafiki baada ya mazungumzo yaliyofanikiwa kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.
Waliozuiliwa, wanaume tisa na mwanamke mmoja, walikuwa wamepelekwa kisiwa cha Farsi, katika Ghuba ya Uajemi, ambako Iran ina kambi ya wanajeshi wa majini.
Wanajeshi wa Revolutionary Guards wamekuwa wakitumiwa kulinda serikali ya Kiislamu ya Iran pamoja na kuzuia uingiliaji kutoka kwa mataifa ya kigeni na kuzuia mapinduzi ya kijeshi na maasi tangu mapinduzi ya 1979.
Taifa hilo huwa pia na wanajeshi wa kawaida ambao hulinda mipaka na kudumisha amani na utulivu ndani ya nchi.
Wanajeshi hao wa Revolutionary Guards wamekuwa wakilinda wa ukali mipaka ya Iran baharini.
Wanabaharia 15 kutoka Uingereza walizuiliwa kwa siku 13 mwaka 2007 baada ya kukamatwa wakiwa eneo la bahari linalozozaniwa kati ya Iran na Iraq.
Licha ya mafanikio makubwa mwaka jana kuhusu mkataba wa nyuklia, uhasama bado umeendelea baina ya Marekani na Iran.

No comments:

Post a Comment