Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
amesema kuwa amefarijika kuona wazee wanapata huduma za matibabu bure na
kwa utaratibu mzuri katika hospitali ya Mkoa wa Ruvuma.
Akizungumza na madaktari, wauguzi
na watumishi wengine wa hospitali hiyo wiki hii, alivyokuwa kwenye
ziara mkoani humo, Waziri Mkuu Majaliwa amesema utaratibu wa kutenga
chumba maalum chenye madaktari wawili mahsusi kwa ajili ya kuwahudumia
wazee unaotekelezwa hospitalini hapo umeondoa adha kubwa kwa wazee
kusubiri matibabu kwa muda mrefu jambo ambalo ni kero kwao.
Amesema kuwa hospitali ya Mkoa
wa Ruvuma imethibitisha kwamba agizo la Serikali la kutaka
hospitali zote za Serikali nchini ziwe na dirisha maalum kwa ajili ya
wazee na watibiwe bure linatekelezeka na kuzitaka hospitali zote nchini
kuiga mfano huo.
“Hospitali zote nchini ziige
mfano wa hospitali ya Mkoa wa Ruvuma kwa kuwaheshimu wazee wanaokwenda
kutibiwa katika hospitali hizo kwa kuanzisha dirisha maalum kwa ajili
yao kama agizo la serikali linavyosema na wasitozwe malipo ya aina
yoyote” alisema Waziri Mkuu.
Aidha, ameongeza kwa kusema kuwa
hata wanapokwenda kuchukuwa dawa uwekwe utaratibu wa kuwapa
kipaumbele kwa kuwahudumia kwanza ili wasisubiri kwa muda mrefu. Na
kusisitiza kuwa kibali maalum kinachowapa fursa wazee kutibiwa bure
hospitalini hapo kindelee kutolewa na kiheshimiwe.
Awali, alitembelea chumba maalum
cha wazee ambapo Waziri Mkuu alipata fursa ya kuzungumza na Bibi
Antonia Moyo ambaye alisema hajawahi kutozwa fedha wala kukaripiwa
wakati wote alipofika hospitalini hapo kwa ajili ya matibabu kupitia
dirisha la wazee.
Waziri Mkuu Majaliwa, pia
ametembelea wodi mbalimbali, chumba cha upasuaji pamoja na duka la dawa
kwa wagonjwa wanaotumia huduma za Bima ya Afya.
No comments:
Post a Comment