Saturday, 9 January 2016

Bomoabomoa kukumba maeneo yote nchini


WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, imewataka wananchi nchini kote waliojenga maeneo ya vyanzo vya maji na hifadhi za misitu kuondoka wenyewe kwa hiari badala ya kusubiri kubomolewa wakati wa opareshani maalumu inayoendelea kufanyika.
Alisema awamu itakayofuata ni ya kushughulika na watumishi wote wa umma ambao wamehusika kwa namna moja ama nyingine kuwasababishia wananchi kupata madhara hayo kwa wao kushindwa kutimiza wajibu wao ipasavyo.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa wizara hiyo, Anjelina Mabula wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na viongozi wa serikali ya mkoa wa Morogoro chini ya Mkuu wa Mkoa huo, Dk Rajab Rutengwe na ule wa wilaya ya Morogoro uliokuwa chini ya mkuu wa wilaya, Muhingo Rweyemamu.
Naibu Waziri huyo alifanya ziara ya siku mbili kuanzia Januari 7, mwaka huu na kupokea taarifa ya mgogoro wa muda mrefu kuhusu ardhi na mipaka ya kijiji cha Mabwegere na vijiji jirani vya Mfulu, Mbigiri na Mambegwa kilichopo wilayani Kilosa na Katibu tawala wa mkoa huo, Eliya Ntandu.
Alisema nyumba zote zilizojengwa kinyume na Sheria ya Mazingira hata kama zilipata vibali kutoka kwenye mamlaka husika kulingana na sheria ya mazingira zinakuwa ni batili na nyumba hizo kukumbwa katika bomoa bomoa.
Mabula alisema ubomoaji wa nyumba zilizojengwa maeneo ya hifadhi na yasiyoruhusiwa kisheria , halitaishia katika Jiji la Dar es Salaam pekee ila litaendelea hadi mikoani na kuwataka wale wote ambao wamejiona wamejenga maeneo yasiyoruhusiwa kuanza kuondoa mara moja pasipo kusubiri opereshani bomoa bomoa iwakute.
Alisema watumishi waliohusika na utoaji wa vibali vya ujenzi katika maeneo ya hifadhi za misitu , vyanzo vya maji na yasiyoruhusiwa kisheria zamu yao ya kuwashughulikia ipo jikoni.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Rutengwe katika hotuba yake fupi ya kumkaribisha Naibu Waziri huyo, alisema kuwa moja ya kero kubwa inayoukabili mkoa huo ni migogoro ya ardhi.
Kwa mujibu wa mkuu wa mkoa, migogoro hiyo inahusu mipaka ya vijiji na vijiji, maeneo ya hifadhi na vijiji, na migogoro ya matumizi ya rasilimali ardhi kati ya wakulima na wafugaji, wananchi na wawezekaji wenye mashamba pori yaliyoendelezwa.

No comments:

Post a Comment