WAKAZI wa Mtaa wa Lingato eneo la Kigamboni, katika Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam na wengine kutoka maeneo mbalimbali ya Jiji, wamevamia eneo la ekari 3,000 na kujikatia maeneo baada ya eneo hilo, lililokuwa la mwekezaji kurudishwa kwa wanakijiji.
Kutokana na hilo, baadhi yao wamemwomba Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kuingilia kati kuzuia uvamizi huo, ambao maofisa wa Ardhi wamethibitisha kuwa wanaofanya hivyo ni wavunjifu wa sheria.
Kaimu Kamishna wa Ardhi ambaye hakutaka kutaja jina, alipozungumza na gazeti hili jana, alisema mambo hayo yanayoendelea hayana kibali kisheria na kwamba uvamizi ni kinyume cha sheria na watachukuliwa hatua.
“Hatuna taarifa hiyo rasmi, lakini kuna mwananchi alipiga simu akasema kuna watu wamevamia ardhi na kugawana… hiyo ni Kisarawe II iko chini ya Manispaa ya Temeke, wao hawana mamlaka ya kufanya wanayofanya,” alisema Kaimu Kamishna huyo.
Kwa mujibu wa wanakijiji wa Lingato na waliotoka maeneo mengine, walidai walifika hapo kwa lengo la kupata ardhi bure baada ya kuelezwa kuwa kijiji hicho kinagawa ardhi hiyo kwa wananchi. Hata hivyo, walilalamikia ugawaji huo kuwa umejaa urasimu.
Katika eneo hilo walikutwa wananchi kutoka sehemu mbalimbali jijini, wakijikatia maeneo na kuweka alama zao huku wakiwa wanalinda maeneo yao wakidai kutotaka urasimu unaoendelea. Baada ya gazeti hili kupata malalamiko hayo na kwenda katika eneo hilo, lilikuta kundi kubwa la watu ambao walikuwa wakielekea huko kujipatia ardhi kama walivyoelezwa, lakini walilalamikia kuwapo na ubabaishaji.
“Hapa tunamtaka aje Waziri wa Ardhi asimamie au atoe mwongozo wa zoezi hili, kumekuwa na urasimu mkubwa watu wanazungushwa bila kupata taarifa sahihi na viongozi hawajulikani ni kina nani,” alisema Athumani Mponda.
Wananchi hao walidai kuna baadhi ya watu wanaojiita wajumbe wa kamati ya ugawaji viwanja hivyo, wamekuwa wakidai fedha kwa watu wanaofika kupata viwanja ingawa walielezwa kuwa viwanja vinatolewa bure.
“Hapa kuna ubabaishaji mkubwa sana, tunaambiwa viwanja vinatolewa bure, lakini tunazungushwa sana karibu wiki mbili tuko hapa tumeandikishwa majina, lakini hatujapewa viwanja na tunaambiwa kuna wengine wanatoa fedha wanapewa,” aliongeza Mponda.
Mwananchi mwingine, Anna Anthoni alisema watu wanaojiita ni wajumbe wa kamati hiyo, wanauza viwanja hivyo Sh 700,000 kwa ekari moja, huku watu ambao hawana fedha wakiendelea kusota.
Nje ya jengo la Ofisi ya Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huo, kulibandikwa fomu ya Ardhi Namba 42 ya kubaini kutelekezwa ardhi hiyo ekari 3,000 bila kufanyiwa makusudio aliyoombea mmiliki wake, Mohamed Akbar.
Tangazo hilo lilielezwa kuwa ardhi hiyo Akbar aliitumia kwa kuchimba mchanga kinyume cha sheria na pia kuwa pori la kujificha majambazi. Nakala ya barua hiyo ya Januari 12, 2016 ilikwenda pia kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Temeke.
Mbali na tangazo hilo, kulikuwa na tangazo lingine ambalo lilieleza kusimamishwa kwa ugawaji mpaka pale kamati itakapotoa tena taarifa kwani kuna eneo ambalo lina zuio la Mahakama.
Hata wakati wananchi wakiwa nje ya ofisi hizo wakisubiri maelekezo, alikuja mtu mmoja ambaye hakutaka kujitambulisha, ambaye aliwakusanya wananchi na kuwaeleza kuwa wanatakiwa kuondoka kama tangazo linavyoeleza kuwa kazi hiyo imesitishwa.
Mtu huyo alisema ardhi ambayo haikuwa na mgogoro, imeshagawiwa kwa wananchi isipokuwa eneo lenye mgogoro mahakamani ambalo tayari kuna majina zaidi ya 1,500 ya watu waliojiandikisha wakisubiri kupata ardhi.
“Eneo limeshafanyika zoezi la ugawaji kwa wenyeji ambao ni wanakijiji hiki na watu wachache ili waweze kupata miundombinu na mambo mengine, wenyeji wetu wamemaliza sasa wanafanya uhakiki wingi wa watu umekuwa mkubwa sana, tuondoke tutapewa taarifa,” alieleza.
Baada ya maelezo hayo, mtu huyo pamoja na watu aliofuatana nao waliondoka wakidai wanaendelea kukagua eneo hilo na kuacha wananchi wakilalamika kutomfahamu na kuhoji kwa nini hapendi kujitambulisha mara zote alizofika hapo ili wamfahamu.
“Huyu mtu sio mara yake ya kwanza kuja hapa, lakini anapokuja anaongea tu, hatumjui ni nani, hii ni dharau kabisa,” alizungumza mwananchi aliyekuwa eneo hilo. Pamoja na kupewa maelekezo hayo, hawakuondoka hapo. Mwandishi wa habari hizi alipojitambulisha kwa mtu huyo na kumuomba amfahamu, hakutoa ushirikiano.
No comments:
Post a Comment