KIMATAIFA

Ndege isiyotumia mafuta yatua Misri

SOLAR IMPULSE
Safari ya kutoka Uhispania ilichukua saa 48
Ndege inayotumia nishati ya jua imetua mjini Cairo, Misri na kupokelewa na waziri na maafisa wengine wa ngazi ya juu wa maswala ya usafiri wa anga wa nchi hiyo.
Ndege hiyo ilikuwa imefanya safari ya saa 48 kutoka mji wa Seville, Uhispania hapo Jumatatu.
Haikutumia mafuta ya ndege ya kawaida hata chembe bali nguvu za kawi zinazotokana na miali ya jua.
Marubani wawili wa Uswizi ndio wanaoiongoza ndege hiyo, huku kituo cha mwisho cha safari hiyo ya majaribio kikiwa Abu Dhabi.
Rubani Andre Borschberg amenukuliwa akisema safari ya saa chache kabla ya kutua mjini Cairo ndiyo ilikuwa na changamoto zaidi kwani kwa mara ya kwanza betri ya ndege hiyo ilikuwa imeshuka hadi asilimia 30 pekee.

Sasa rubani Bertrand Piccard ndiye atachukua usukani wa mkondo wa mwisho wa safari hadi Umoja wa Milki za Kiarabu lakini haijajulikana mkondo huo utachukua muda gani kwani itategemea zaidi hali ya hewa.
Huko ndiko mpango huo wa majaribio wa ndege hiyo ya sola ulianza hapo 2015.
Marubani hao Piccard na Borschberg awali walikuwa wakifanyakazi katika mradi wa sola uitwao Solar Impulse kwa muda wa zaidi ya miaka 10.
Japo ni safari ya polepole ndege hiyo imeweza kuvuka anga zaidi ya nchi 7 nyinginezo zikiwa ni zile zilizo na shughuli nyingi za ndege za usafiri wa umma.
Ni mradi ambao kufikia sasa umegharimu $100 millioni, tangu 2002 lakini lengo la utafiti huu ni kuwa huenda hatimaye gharama kama hiyo itakuwa ndogo ikilinganishwa na gharama ya harakati za kukabiliana na changamoto za kuongezeka kwa hali ya uchafuzi wa hewa kutokana na usafiri wa ndege nyingi unaotumia kawi ya mafuta.

Gari lenye kasi zaidi duniani kuundwa


Mradi wa kuunda gari liendalo kasi Zaidi duniani umefufuliwa na gari hilo linatarajiwa kujaribu kuvunja rekodi ya dunia mwaka ujao.
Mpango wa kuunda gari hilo lililopewa jina Bloodhound ulikwama miezi ya karibuni kutokana na matatizo ya kifedha.





Lakini mfadhili mpya amepatikana na wahandisi wanaweza sasa kkurejelea kazi ya kulitengeneza.
Oktoba 2017 itakuwa miaka 20 tangu kuwekwa kwa rekodi ya sasa ya kasi ya gari ardhini ambayo ni kilomita 1,228 kwa saa (763mph).
Rekodi hiyo iliwekwa na gari lililopewa jina Thrust SSC jangwani Marekani.

 



Wanaounda Bloodhound wanatarajia gari hilo liweze kufikia kasi ya hadi kilomita 1,287 kwa saa nchini Afrika Kusini.
Gari hilo linaundiwa Uingereza.
Gari hilo liliwasilishwa kwa maonesho Canary Wharf, London likiwa bado halijakamilika mwezi Septemba mwaka jana.




Tangu wakati huo, limekuwa Bristol likiwa halifanyiwi kazi yoyote.
Gari hilo litatumia injini ya ndege aina ya Eurofighter-Typhoon ambayo itaundwa na kampuni ya Nammo ya Norway.
Gia yake itaundwa na wahandisi wa mradi huo wa Bloodhound na pampu yake itakuwa ya Jaguar V8.
Litafanyiwa majaribio Cornwall, Uingereza mwezi Mei au Juni mwaka ujao.

Mbunge wa Afrika Mashari Auawa Kikatili Burundi

MBUNGE wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kutoka nchini Burundi, Hafsa Mossi, ameuawa na watu wasiojulikana kwa kupigwa risasi katika mji mkuu wa Bujumbura.

Mossi aliyewahi kuwa Waziri wa Masuala ya Afrika Mashariki katika serikali ya nchi hiyo, aliuawa jana katika barabara ya Gihosha eneo la Nyankoni.

Taarifa zilizothibitishwa na Msemaji wa Polisi wa nchi hiyo, Pierre Nkurikiye zilisema kuwa mauaji hayo yalifanyika saa 4:00 asubuhi. Nkurikiye alisema mbunge huyo alipigwa risasi kifuani kwenye moyo na kukimbizwa katika Hospitali ya Jeshi ya Kamenge ambako baadaye alipoteza maisha.

EALA ni chombo cha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambacho wanachama wake ni Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini, ukiwa ni umoja wa kikanda wenye ushirikiano wa kibiashara huku ukikusudia kuwa na sarafu moja na shirikisho moja la kisiasa.

Mkazi wa eneo alikouawa Mbunge huyo, Achel Majabuka alisema kuwa alisikia mlio wa risasi na baadaye kuona watu wawili wakiondoka katika gari baada ya kuwatishia kwa silaha wakazi wa eneo hilo.

Kwa upande wake, Bunge la Afrika Mashariki katika taarifa yake iliyotolewa Kampala nchini Uganda, ilisema kuwa Mossi ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Wabunge wa Burundi katika EALA, alipigwa risasi katika eneo la Mulanga Mashariki mwa Bujumbura.

Alimkariri msemaji huyo wa Polisi akieleza kuwa Mossi aliuawa karibu na nyumbani kwake, huku Mbunge mwingine wa Burundi katika EALA, Emerence Bucumi akithibitisha kifo hicho.

Spika wa Bunge la Afrika Mashariki, Daniel Kidega alilaani mauaji hayo na kumuelezea Mossi kuwa ni mchapakazi aliyekuwa amejikita kusimamia na kutetea utengamano wa ukanda huo.

Spika huyo ambaye yuko Uganda kwa ziara ya kikazi, ameishauri Serikali ya Burundi kuwatia nguvuni mara moja wauaji wa Mossi ambaye pia aliwahi kuwa Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).

“Ninatoa salamu za rambirambi kwa serikali, familia, marafiki na wananchi wa Burundi. Ninawaomba wawe watulivu katika wakati huu mgumu na ninaamini mamlaka husika zitafanya kazi kwa haraka kuhakikisha waliohusika na tukio hilo la kinyama wanatiwa nguvuni mara moja,” alisema Spika Kidega.

Kwa upande wake, Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza alikielezea kifo cha mwanasiasa huyo kuwa ni cha kudharauliwa kwa serikali yake. Naye Katibu Mkuu wa EAC, Balozi Liberat Mfumukeko, alisema amesikitishwa na kifo hicho cha Mbunge huyo aliyeeleza alikuwa rafiki na dada na kuwa jumuiya imepoteza mwakilishi aliyekuwa akifanya kazi bila kuchoka.

Mwaka jana, Mossi alitembelea wakimbizi wa Burundi nchini Rwanda na kulia, ameuawa wakati mazungumzo kuhusu mgogoro wa Burundi yakiwa yanaendelea kufanyika jijini Arusha.

Alikuwa na Shahada ya Uandishi wa Habari na aliwahi kufanya kazi katika BBC na alikuwa Waziri wa Burundi wa Masuala ya Afrika Mashariki hadi Juni 2012 alipochaguliwa kuwa Mbunge wa EALA.

Pia, aliwahi Waziri wa Mawasiliano, Habari, Mahusiano na Bunge na Msemaji wa Serikali ya Burundi kuanzia mwaka 2005 hadi 200

Ndege ya kisasa ya Ethiopia yatua Kenya

Airbus A350 XWB
Ethiopia Airlines ndiyo ya kwanza Afrika kununua ndege aina ya Airbus A350 XWB
Ethiopia imekuwa taifa la kwanza barani Afrika kununua ndege ya kisasa aina ya Airbus A350 XWB.
Ndege hiyo, Airbus A350, ndiyo ya hivi karibuni kuzinduliwa na kampuni ya ndege ya Airbus ya Ufaransa.
Ndege hiyo, iliyo na uwezo wa kubeba zaidi ya abiria 300, ilitua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi Kenya Jumatano jioni ikitokea mjini Addis Ababa, Ethiopia.


 


"Ndege hii ya kisasa itasaidia katika utoaji wa huduma zetu, kuimarisha mtandao wetu wa usafiri, na kupunguza kwa kiasi kikubwa viwango vya hewa chafu inayotolewa wakati wa usafiri wa ndege,” Mkurugenzi mkuu wa shirika la Ethiopian Airlines Tewolde GebreMariam amesema.
Ndege hiyo ni ya kwanza kuwasilishwa kwa kampuni hiyo, huku nyingine 13 ilizoagiza kutoka kwa kampuni ya Airbus zikisubiriwa hivi karibuni.
Safari ya kwanza ya ndege hiyo ilifanyika tarehe 2 Julai iliposafiri kutoka Ufaransa hadi mjini Lagos, Nigeria.
 


Viwango vya juu vya teknolojia iliyotumika kuunda ndege hiyo, vinachangia katika kuinua utendakazi wake, kupunguza matumizi ya mafuta pamoja na kupunguza kwa kiasi kikubwa utoaji wa hewa chafu.
Kampuni ya Ethiopian Airlines inaorodheshwa ya kwanza barani Afrika kwa faida na pia idadi ya maeneo inayosafirisha abiria.


Mwaka wa 2012, shirika hilo pia lilikuwa la pili duniani na la kwanza barani afrika kununua ndege aina ya Boeing 787 Dreamliner, ya kampuni ya Boeing, yenye afisi zake kuu Chicago, Marekani.


Kampuni ya Airbus na Boeing zinaongoza duniani katika utengenezaji wa ndege za kisasa, japo Airbus ina umaarufu mkubwa na imeipiku Boeing kwa faida na uuzaji wa idadi kubwa ya ndege.7.

Burundi, taifa katika Afrika Mashariki imekumbwa na ghasia na vifo kwa zaidi ya mwaka sasa.

Mgogoro huo wenye kuendana na umwagaji damu, umesababisha watu 1,500 kuuawa, huku ukiwahusisha wafuasi wa Rais Nkurunziza na wale wanaopinga ushindi wake wa uchaguzi wa Julai, 2015 kwa mara ya tatu, wakidai kuwa ulikiuka Katiba ya nchi hiyo



No comments:

Post a Comment