Wednesday, 13 July 2016
Mambo 5 Yanayokuzuia Kufikia Mafanikio Makubwa
Kuna mambo mengi tunayoweza kuyazungumza ikiwa kama sehemu ya vikwazo vinavyokuwa sababu kubwa ya kuwarudisha watu wengi nyuma na kushindwa kufikia mafanikio makubwa ya kutimiza maono na ndoto walizonazo katika Maisha yao hapa duniani. Lakini leo nataka tuangalie baadhi ya Mambo makuu matano ambayo yamekuwa sugu kwa watu wengi na kuwazuia kufikia malengo na mipango yao kila mwaka na kila wakati wanapotaka kufanya hivyo na hasa kwa mambo makubwa yenye matokeo makubwa na mazuri kwao.
Nataka ufahamu makala hii ipo kwa ajili yako wewe uliye na ndoto au maono makubwa kwa muda mrefu na umekuwa sehemu ya kusema kila wakati utafanya au utaanza kutekeleza maono yako hayo mazuri uliyonayo, lakini hadi sasa umeshindwa kufanya hivyo kutokana na sababu ambazo hata wewe mwenyewe hujui au yawezekana unazijua lakini umeshindwa kufahamu ni namna gani ya kutoka katika hali hiyo ya kutokufanikisha maono hayo.
Yawezekana una maono ya kufungua kampuni kubwa ya kuuza bidhaa au kutoa huduma, au unahitaji kuongeza wateja wengi zaidi katika biashara yako, au unahitaji kwenda kusoma nje na kuongeza ujuzi mpya wa eneo la taaluma unayoipenda, au unataka kuanza kufundisha na kufanya semina za mafunzo ukiwa kama muhamasishaji, au unahitaji kutengeneza mtandao wa mahusiano na mtu fulani mkubwa mwenye uwezo kiuchumi, nakadhalika.
Katika yote hayo na mengine mengi zaidi ambayo sijayataja katika makala hii na hapo juu; yawezekana mojawapo ni sehemu ya ndoto ya maisha yako uliyonayo moyoni mwako, lakini umeshindwa kujua ni namna gani ya kuifanya iwe sehemu halisi ya muonekano katika dunia hii ili kila mmoja apate kuiona na kupata sehemu ya matunda yake. Unazani ni kwa nini umekuwa mwoga wa kutimiza ndoto yako uliyonayo.
Je, ni mambo gani unayozani yanakufanya uogope kutimiza ndoto yako uliyonayo? Naamini kila mmoja ukimuuliza swali hili atakupa majibu yake kulingana na kila mmoja kutofautiana na mwingine kwa kila eneo fulani. Kumbuka unaposhindwa kutimiza ndoto au maono yako uliyonayo, maanake unashindwa au unazuia kufikia mafanikio makubwa unayoyahitaji katika maisha yako.
Zipo sababu na mambo matano makuu ambayo ndio sababu kubwa inayowafanya watu wengi kushindwa kufikia ndoto na maono yao waliyonayo na zaidi sana katika kufikia mafanikio makubwa. Hata kama kila mmoja ana sababu binafsi zinazomfanya kushindwa kutimiza ndoto aliyonayo, lakini zipo sababu ambazo zimekuwa hazina maana ya msingi kwa wengi na ni sababu sugu kwa watu wengi katika kutimiza ndoto zao na kufikia mafanikio makubwa.
Sababu au Mambo hayo matano ambayo yamekuwa sugu pasipo kujua au kwa kujua kwa watu wengi, nimeamua kukuandikia hapa ili uweze kujipima na kufahamu kama na wewe binafsi ni miongoni mwa watu walio katika kifungo cha mambo haya, na namna gani unaweza kutoka katika kifungo cha sababu hizi zinazokupelekea kutokufikia mafanikio makubwa unayoyahitaji.
Mambo hayo matano ni kama ifuatavyo; soma na uamue kubadilika moja kwa moja pasipo kurudi nyuma, tena kwa kutekeleza ushauri huu ninaokupa kwa haraka ili ufikie kufanya kile ambacho ni ndoto yako itakayokupelekea kufikia kuwa na mafanikio unayotaka.
Jambo la Kwanza:
Hofu.
Ndio. Hofu. Nataka nikuambie hofu ni sababu kubwa inayokufanya usitimize ndoto yako na inayowafanya watu wengi kushindwa kufikia mafanikio makubwa katika maisha yao hapa duniani. Kumbuka ukiwa na hofu huwezi kufanya au kutekeleza jambo lolote lile unalohitaji kulifanya, hasa kama ni malengo au mipango uwe na uhakika inakufa tu pale unapokuwa unatanguliza kuwa na hofu ya kutekeleza malengo yako husika. Hofu ya kujaribu, hofu ya kufanya au kutekeleza na hofu ya kuogopa watu.
Kuna madhara mengi na makubwa ya hofu na mojawapo ni kuua ujasiri na nguvu ya utekelezaji ndani ya mtu (nguvu ya ku-focus). Lakini pia hofu inapunguza kasi ya kuyafikia malengo yako uliyojiwekea, hofu ni mlango mkubwa wa kuingiza maadui wengine wa kukuzuia katika safari yako ya mafanikio kama vile magonjwa, nakadhalika.
Kama unahitaji kufikia ndoto na maono yako makubwa uliyonayo hauna budi kuondokana na hofu inayokuzuia kufanya hivyo.Ushauri wangu kwako ili uondokane na hofu ni vizuri ujenge tabia ya kujiamini katika kile unachokihofia. Jenga kujiamini binafsi (self-confidence) katika jambo unaloogopa kulifanya na jitie nguvu kulifanya pasipo kuangalia mazingira yaliyokuzunguka na yanayokujengea hofu hiyo.
Tabia nyingine kubwa na nzuri ya kujenga ujasiri ni kusoma au kutafuta ufahamu wa kutosha au kujifunza zaidi juu ya eneo linalokujengea hofu kulitekekeleza au kulifanya. Jifunze zaidi kwa kusoma vitabu mbali mbali vinavyotoa siri ya kuondokana na hofu na uoga na kukupa mbinu za namna ya kujenga ujasiri na kujiamini
Jambo la Pili:
Uvivu na Usingizi mwingi.
Nataka nikuambie sababu hii ni kweli na wala si kinyume kama vile unavyozani. Nimeona watu wengi wameshindwa kutimiza ndoto zao kwa sababu ya kuendekeza vitu vidogo sana na mojawapo ni kama hili la kuwa na uvivu wa kujibidiisha kufanya jambo fulani linalowaletea mafanikio katika maisha yao.
Unaweza kuona jambo hili ni kama jambo dogo sana katika kukuzuia kufikia mafanikio makubwa, lakini nataka nikuambie jambo hili si jambo dogo kama unavyozani katika kichwa na moyo wako. Uvivu na usingizi ni mojowapo ya vyanzo vikubwa vya kuzuia mafanikio ya watu wengi na hasa kwa vijana wa leo. Vijana wengi wanatamani kuwa matajiri na watu wenye mafanikio makubwa kama watu wengine fulani katika jamii, lakini wengi wao wameshindwa kufikia hapo kutokana na tabia halisi iliyowakamata ya kuendekeza uvivu na kutokufanya kazi kwa bidii.
Huwezi kufanikiwa nje ya kujituma na kufanya kazi kwa bidii kubwa katika maisha yako. Nje ya hapo uwe na uhakika utajiingiza kupata mali au utajiri husio wa halali na wa kweli, na hatimaye hautofikia popote zaidi sana ya kujishushia hadhi yako. Ndio. Kujishushia hadhi yako. Leo tunaona watu wanafanikiwa kumbe ni wauza madawa ya kulevya, wakwepa kodi katika serikali, wala rushwa na ufisadi, nakadhalika. Hii ni sababu ya kutokuwa waaminifu na wanahitaji utajiri wa haraka pasipo kutaka kulipa gharama zaidi.
Acha uvivu na usingizi husio wa muhimu katika maisha yako, hasa kwako wewe kijana. Jitume na kufahamu umuhimu wa ndoto yako katika jamii yako, ndoto yako ni msaada tosha katika kuisaidia jamii yako kuendelea kiuchumi zaidi pale utakapoinuka na kuitimiza.
Jambo la Tatu:
Ubinafsi.
Hili nalo ni chachu kubwa ya kufanikiwa kwa watu wengi, na hasa kwa upande wetu waafrika limekuwa ni tatizo kubwa kuanzia katika nganzi za uongozi wa kitaifa, mashirika na makampuni yetu tuliyonayo, hadi kwa watu binafsi. Ubinafsi umekuwa ni chanzo kikubwa cha kubana mawazo yetu mazuri tuliyonayo hata katika kusaidia wengine kufanikiwa.
Wapo watu wana hofu ya kushirikisha watu wengine mambo yao au ndoto zao walizonazo ili kupata msaada wa ushauri kutoka upande wa pili. Hii wakati mwingine inaweza kuwa ni nzuri kwa upande mmoja na upande mwingine kuwa mbaya, kutokana na tabia ya ubinafsi ndani ya mtu ambayo inaweza kuwa na faida chanya au faida hasi kwake. Usipende kukaa na kitu ndani yako tafuta mshauri mwema unayemwamini na kumwomba ushauri juu ya jambo unalotaka kulifanya ili akujenge kimawazo. Nje ya hapo hautoweza kutoka na kufanikiwa kutokana na kujifungia kimawazo badala ya kutafuta ushauri utakaokujenga.
Jambo la Nne:
Kukosa Maarifa na Ufahamu wa kutosha.
Jiulize umesoma vitabu vingapi tangu mwaka huu uanze, umeuzulia semina ngapi, au umesikiliza na kuangalia mafundisho mangapi, nakadhalika. Kila mtu ana eneo lake analohitaji kujifunza kila siku ili awe bora zaidi katika eneo hilo na kubobea ili kumsaidia kufanya mambo kwa ufanisi na uahakika zaidi.
Watu wengi wameshindwa kutekeleza malengo na mipango yao waliyonayo wakati mwingine kwa sababu kukosa ufahamu au taarifa sahihi juu ya eneo wanalotaka kufanikiwa. Kwa mfano kama hauna taarifa sahihi za kuwekeza katika madini au gesi huwezi kufanya hivyo hadi upate ufahamu wa kuanza kufanya hivyo, nje ya hapo utajikuta ukitafuta mtu wa kukusaidia kufanya hivyo lakini kwa malipo makubwa. Unaona ni jinsi gani maarifa na ufahamu vilivyo vya muhimu katika kukusaidia kufanikiwa katika malengo na mipango yako uliyonayo? Tafuta maarifa ili uweze kufikia mafanikio makubwa juu ya eneo unalotaka kufanikiwa.
Ukikosa maarifa unaweza kukosa au kupitwa na fursa fulani nzuri zinazopita mbele yako. Maariafa ni muhimu kuliko fedha na dhahabu zote zilizojaa kwenye chumba kimoja wanachog’ombania watu wengi. Tafuta maarifa zaidi ili uzidi kuona fursa nyingi zaidi wasizoziona wengine.
Jambo la Tano:
Aina wa watu ulionao au waliokuzunguka.
Fanya zoezi hili leo kwa hapo ulipo iwe ni ofisini, kazini kwako, kwenye biashara, chuoni, nyumbani, nakadhalika. Angalia watu waliokuzunguka wana mawazo gani dhidi ya maisha yao binafsi, jamii yao na watu wengine. Kama umezungukwa na watu wenye mawazo hasi kwa muda mrefu sana badala ya watu wenye mawazo chanya uwe na uhakika kwa namna hiyo upo kwenye shida na hatari ya kushindwa kutimiza ndoto na maono yako uliyonayo.
Huwezi kufanikiwa kwa kiwango cha juu kama binafsi utakuwa miongoni mwa watu wanaotamka kushindwa muda wote, kuwa miongoni mwa wale wanaoona maisha ya mafanikio hayaji pasipo kwenda kwa mizimu na kutambikia, kuishi katikati ya watu wenye kuzungumza tu pasipo vitendo, nakadhalika.
Nataka nikuambie watu waliokuzunguka wana mchango mkubwa sana katika kukufanya wewe ufanikiwe au ushindwe kufanikiwa katika maisha ya ndoto yako uliyonayo. Kama umezungukwa na watu chanya uwe na uhakika utakuwa na nafasi kubwa na nzuri ya kufikia katika hatima ya ndoto yako, lakini kama utakuwa miongoni mwa mkondo wa watu wenye mtazamo hasi kuhusu maisha yao na mafanikio ni lazima usipokuwa mwangalifu utashindwa kufikia mafanikio unayoyahitaji.
Hadi hapo kazi ni kwako kuchukua hatua ya wewe kuamua kubadilika au kutokubadilika, ni uamuzi wako kufanya hivyo. Nami natamani uwe sehemu ya wale watakaochukua hatua ya kubadilika dhidi ya yote uliyoyasoma na kujifunza hapa. Utafikia malengo na mipango yako mikubwa uliyonayo kama ukiamua kuachana na hofu, uvivu, ubinafsi, kutokupenda kujifunza na kuwa mbali na watu wenye mawazo hasi.
Nakutakia mafanikio mema na maisha mazuri ya kutumikia ndoto na maono yako uliyonayo katika maisha yako hapa duniani. Kwa mawasilino na ushauri zaidi wasiliana nasi kupitia njia zifuatazo:
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment