RAIS wa Argentina Mauricio Macri na Lejendari wa Nchi hiyo Diego Maradona wamemtaka Lionel Messi kuendelea kuichezea Nchi yao baada ya Jana kutangaza kujiuzulu.
Jana Messi alikosa Penati ya Kwanza katika Mikwaju Mitano Mitano ya Penati ambayo iliipa ushindi Chile kwa Penati 4-2 na kutwaa Copa America Centenario.
Mara baada ya Mechi hiyo, Messi, ambae ni Mchezaji Bora Duniani mara 5 na ambae hajatwaa Taji lolote kubwa na Argentina, alitangaza kujiuzulu.
Akiongea baada ya Mechi hiyo Messi alisema: "Haya hayakupangwa kwangu. Kwangu mimi Timu ya Taifa imekwisha. Nimefanya kila niwezalo na inauma sana kutokuwa Bingwa."
Messi, mwenye Miaka 29, alianza kuichezea Argentina Mwaka 2005 na kucheza Mechi 115 ambapo Juzi alivunja Rekodi ya Ufungaji Bora Argentina ya Gabriel Batistuta kwa kupachika Bao 55.
Lakini ukiachia Medali ya Dhahabu ya Olimpiki aliyotwaa Mwaka 2008, Messi hajatwaa Taji lolote huku Argentina ikibwagwa katika Fainali kubwa 4.
Kuanzia 2014, Argentina na Lionel Messi, Mchezaji Bora Duniani mara 5, wamefika Fainali 3 na zote kufungwa.
2014 walicheza Fainali ya Kombe la Dunia huko Brazil na kufungwa na Germany 1-0 na Mwaka Jana kutolewa kwa Penati na Chile huko Santiago kwenye Copa America.
Leo Alfajiri huko USA, kwenye Fainali ya Copa America Centenario, Argentina na Chile zilitoka 0-0 katika Dakika 120 za Gemu na Gemu kuamuliwa kwa Mikwaju ya Penati.
Lakini Jana hiyo hiyo Rais wa Argentina, Mauricio Macri, alimtafuta Messi na kuongea nae ili abaki kuichezea Nchi yake.
Nae Lejendari Diego Maradona amesisitiza Lionel Messi hapaswi kufuata uamuzi wake wa kujiuzulu kuichezea Argentina.
Maradona, ambae alitwaa Kombe la Dunia Mwaka 1986 akiichea Argentina na pia kuwa Kocha wake kati ya 2008 na 2010, amemtaka Messi kubaki na kucheza Fainali za Kombe la Dunia za Mwaka 2018 huko Russia.
Maradona amesema: “Messi lazima abaki Timu ya Taifa. Aende Russia akiwa na fomu ya Bingwa!”
No comments:
Post a Comment