UTANGULIZI
1.
Mheshpika, naomba
kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu lipokee, lijadili na kupitisha Makadirio ya
Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17.
Pamoja na hotuba hii, ninawasilisha vitabu
vinne vinavyoelezekina makadirio ya Bajeti. Kitabu cha Kwanza ni
Makadirio ya Mapato; Kitabu cha Pili ni Makadirio ya Matumizi ya Kawaida
kwa Wizara, Idara za Serikali zinazojitegemea, Taasisi na Wakala za Serikali;
Kitabu cha Tatu ni Makadirio ya Matumizi ya Kawaida kwa Mikoa na Mamlaka
za Serikali za Mitaa; na Kitabu cha Nne ni Makadirio ya Matumizi ya
Maendeleo kwa Wizara, Idara za Serikali zinazojitegemea, Taasisi na Wakala za
Serikali, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, upo
Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2016 pamoja na Muswada wa Sheria ya kuidhinisha
matumizi ya Serikali wa mwaka 2016 ambayo ni sehemu ya Bajeti hii.
2.Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa napenda kumshukuru Mungu kwa
baraka na amani anayoendelea kuijalia nchi yetu na pia kwa kuniruhusu kusimama
hapa mbele ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwasilisha Bajeti ya
Serikali kwa mwaka 2016/17. Aidha, kwa namna ya pekee nachukua fursa hii
kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa
Makamu wa Rais na mwanamama wa kwanza kushika nafasi hiyo katika historia ya
nchi yetu.
Nampongeza pia Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, kwa kuchaguliwa
tena kuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Vilevile, nampongeza
Mheshimiwa Kassim M. Majaliwa kwa kuchaguliwa na wananchi wa jimbo la Ruangwa
kuwa Mbunge wao na kuteuliwa na Mhe. Rais na kuthibitishwa na Bunge kuwa Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Napenda pia kukupongeza wewe
Mheshimiwa Spika pamoja na Naibu Spika kwa kuchaguliwa kuongoza Bunge letu
Tukufu. Kadhalika, natumia fursa hii
kumpongeza Mhe. Mohamed Othman Chande, Jaji Mkuu wa Tanzania, kwa kuongoza
mhimili wa Mahakama kwa weledi mkubwa.
3.Mheshimiwa Spika, niruhusu pia
niwashukuru sana waheshimiwa wenza wa viongozi wetu wa kitaifa: Mama Janet
Magufuli, Bwana Ameir Hafidh Ameir (mume wa Mhe. Makamu wa Rais), Mama
Mwanamwema Shein, Mama Mary Majaliwa, Mama Fatuma Ramadhani Mganga (mke wa Mhe.
Spika), Bwana James Andilile (mume wa Mhe. Naibu Spika) na Mama Saada El-Maamry
Othman (mke wa Mhe. Jaji Mkuu) kwa kuwasaidia na kuwatunza viongozi wetu
vizuri. Asante kwenu wote na Mungu
awabariki.
4.Mheshimiwa Spika, kwa mara nyingine
natoa shukrani za pekee kwa Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniteua kuwa Mbunge na Waziri wa Fedha na
Mipango. Ninatambua kwamba wananchi wa Tanzania wananidai! Tarehe 29 Februari, 1968
Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwasilisha hati ya
madai kama ifuatavyo, nanukuu: “Tunadai
nini basi kwa wale wenzetu waliojaliwa kupata elimu? Tunadai huduma kwa
wananchi na huduma ambayo ukubwa wake utalingana na kiasi cha elimu waliyoipata”
mwisho wa kunukuu.
Hivyo, napenda kumuahidi tena Mhe. Rais na Watanzania kwamba
nitaibeba dhamana hii kwa bidii na uadilifu ili kulipa deni langu kwa nchi
yangu. Vilevile, nawapongeza waheshimiwa Wabunge wote kwa kuchaguliwa kwenu na
kuwa sehemu ya Bunge hili. Napenda pia
kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri wenzangu na Naibu Mawaziri kwa dhamana kubwa tuliyopewa
na Mheshimiwa Rais kuwatumikia Watanzania.
Nampongeza pia Dkt. Thomas
Kashililah, Katibu wa Bunge na Bw. Hussein Kattanga, Mtendaji Mkuu wa Mahakama
kwa kuratibu vyema shughuli za Bunge na Mahakama kwa mtiririko huo. Napenda pia
kumpongeza Prof. Mussa Assad, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
kwa kazi nzuri anayoifanya ya kukagua na kutoa taarifa za matumizi ya fedha za
umma kwa wakati.
5.Mheshimiwa Spika, ninaishukuru sana
Kamati ya Bunge ya Bajeti chini ya uenyekiti wake Mhe. Hawa Abdulrahman Ghasia,
Mbunge wa Mtwara vijijini na Makamu Mwenyekiti Mhe. Josephat Sinkamba Kandege,
Mbunge wa Kalambo, kwa kuchambua kwa kina bajeti za Mafungu yote na kutoa
mapendekezo na ushauri.
Aidha, napenda kuwashukuru wenyeviti wa kamati za
kisekta kwa ushauri na mapendekezo waliyotoa wakati wakichambua rasimu ya
Bajeti hii. Ninamshukuru pia Mhe. George Mcheche Masaju (Mb), Mwanasheria Mkuu
wa Serikali kwa kutayarisha kwa wakati Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2016
na Muswada wa Sheria ya Matumizi wa mwaka 2016 ambayo ni sehemu ya Bajeti hii.
6.Mheshimiwa Spika,
napenda kumpongeza
Mhe. Dkt. Ashatu Kachwamba Kijaji, Mbunge wa Jimbo la Kondoa kwa kuteuliwa kuwa
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango na pia ninamshukuru kwa ushirikiano
anaonipatia katika utekelezaji wa majukumu yangu.
Aidha, napenda kumshukuru
Dkt. Servacius B. Likwelile, Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango kwa
uratibu na usimamizi mzuri wa maandalizi ya Bajeti hii. Kadhalika, nawashukuru
Naibu Makatibu Wakuu; Gavana wa Benki Kuu; Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania; Msajili wa Hazina; Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu;
Wakuu wa taasisi zilizo chini ya Wizara; Wakuu wa idara, vitengo na Watumishi
wote wa Wizara na taasisi zake kwa kazi kubwa waliyoifanya kukamilisha Bajeti
hii.
7.Mheshimiwa
Spika,
Bajeti hii imezingatia mawazo na mapendekezo ya wadau mbali mbali wakiwemo
wenye viwanda, wafanyabiashara na wengine wengi. Nawashukuru wote kwa mawazo na
ushauri wao. Kipekee niwashukuru wajumbe wa kamati ya wataalamu na ushauri wa
masuala ya kodi (Task Force) na kamati ya kitaifa ya ushauri wa kodi (Think
Tank) kwa ushauri wao mzuri walionipa.
No comments:
Post a Comment