Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Boniface Jacob amebaini matumizi ya Sh392
milioni zilizoandikwa kwenye taarifa ya manispaa hiyo kuwa zimetumika
kwa ajili ya ukarabati wa barabara ya Sinza - Igesa ambao haukufanyika.
Katika taarifa ya manispaa hiyo, fedha hizo zilidaiwa kutumika kwa ajili ya matengenezo ya mara kwa mara ya barabara hiyo.
Akizungumza
kwenye ziara ya Kamati ya Uchumi na Fedha ya Manispaa hiyo, Jacob
alisema ni ajabu kuona hakuna matengenezo yoyote yaliyofanyika kama
taarifa hiyo inavyoelezwa huku fedha zikionekana kulipwa.
Alisema
hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayebainika kuhusika
kwenye matumizi hayo huku akiiomba Taasisi ya Kupambana na Kuzuia
Rushwa (Takukuru) kuchunguza matumizi ya fedha hizo.
“Fedha
hizi zinaonekana zimelipwa kwa mkandarasi Skol Building Contract Ltd
wakati barabara ina mahandaki na mashimo makubwa, ikionyesha kwamba
haijakarabatiwa,” alisema.
Alisema kama wasingeamua kukagua
thamani ya fedha za halmashauri hiyo zinavyotumika kwenye miradi hiyo
katika kipindi cha Jaruari hadi Machi mwaka huu wasingegundua
udanganyifu huo.
Meya huyo aliyeonyesha kukasirishwa na hali
hiyo, aliwataka wataalamu wa halmashauri hiyo waliohusika kuandika
ripoti hiyo kutoa maelezo ya kina kuhusu udanganyifu huo.
“Hivi
kama tungenyamaza tusiamue kukagua miradi hii nani angesimama kueleza
hayo? Mnaleta hadithi wakati tayari mmeshalidanganya Baraza la Madiwani
kwamba fedha hizi zimetumika kukarabati barabara hii?” alisema.
Akitetea
matumizi ya fedha hizo, mchumi wa manispaa hiyo, Huruma Eugen alisema
zilizoandikwa kwenye taarifa hiyo zimetumika kwa ajili ya kulipa madeni
ya nyuma.
Huku kukiwa na mabishano baina yake na Meya, Eugen
alisema awali, ujenzi wa barabara hiyo ulifanyika kwa kukopa kutoka
fedha za Mfuko wa Barabara, jambo lililowafanya watumie fedha za mapato
ya ndani ya halmshauri kulipa deni hilo.
“Hela ilitoka kwenye mfuko wa
barabara na imerudishwa kwenye akaunti, japo huku imeandikwa imelipwa
kwa mkandarasi aliyejenga barabara hii,” alisema Eugen.
Hata
hivyo, Meya huyo alisema kama fedha hizo zimetumika kwa ajili ya kulipa
madeni zingeonyesha wazi kwenye taarifa hiyo badala ya kuandikwa kwamba
zimeelekezwa kwenye ukarabati wa barabara, wakati jambo hilo
halijafanyika.
Diwani wa Sinza, Godfrey Chindaweli alieleza
kushangazwa na taarifa inayoonyesha ukarabati wa barabara hiyo wakati ni
miongoni mwa barabara zenye mashimo kwenye kata yake.
Alisema
mara kadhaa amepokea malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu ubovu wa
barabara hiyo na kuahidi kuikarabati akidhani ipo kwenye mpango.
“Nimeshangaa
kuona miongoni mwa miradi iliyotumia fedha za robo ya tatu ya mwaka huu
wa fedha, barabara ya Sinza ambayo haijaguswa ipo kwenye orodha, jambo
hili linahitaji majibu ya haraka,” alisisitiza.
Diwani wa
Makongo, Ndeshukuru Tungaraza aliwataka wataalamu wa halmashauri hiyo
kueleza ilikuwaje fedha ziandikwe kwamba zimetumika kwa ajili ya
ukarabati wa barabara wakati hazikutumika kwa kazi hiyo.
Tungaraza
alisema hakuna sheria ya matumizi ya fedha inayoelekezwa kufanya kama
ambavyo manispaa hiyo imefanya, jambo ambalo madiwani hawatakubaliana
nalo.
Katika eneo la Mwananyamala kwenye Barabara ya Akachube
inayoelekea kwenye kituo cha daladala cha Makumbusho, Meya huyo
aliwaagiza wahandisi aliowakuta wakiendelea na ujenzi kukamilisha haraka
ili kuondoa usumbufu kwa watumiaji wa barabara hiyo.
Alisema malalamiko mengi ya wananchi kuhusu ubovu wa barabara yanatokana na uzembe wa kutosimamia kwa ukamilifu miradi iliyopo.
Hata
hivyo, mkandarasi wa kampuni ya Delmonto, Rajab Athman alisema
wanashindwa kukamilisha kwa wakati barabara hiyo kutokana na kupasuka
kwa mabomba ya maji.
“Maji yanamwagika mengi, hivyo tunawasubiri
Dawasco wakishakamilisha kutengeneza mabomba yaliyopasuka tutaendelea
kujenga,” alisema.
Katika ujenzi wa Jengo la Bima
ya Afya, katika Hospitali ya Mwananyamala linaloendelea kujengwa, Meya
Jacob alionyesha wasiwasi wa jengo hilo kukamilika mapema kabla mpango
wa matumizi ya bima kwa wananchi wote kuanza.
“Mpango huu
unatarajia kuanza Julai lakini mpaka sasa hali inaonyesha halitakamilika
kwa wakati, jambo hili linanipa wasiwasi,” alisema.
No comments:
Post a Comment