Wednesday, 18 May 2016

Mganga mbaroni akidaiwa kugoma kumhudumia mjamzito


Polisi mkoani Mara inamshikilia mganga wa zahanati katika Kijiji cha Rwamchanga wilayani Serengeti kwa madai ya kushindwa kumhudumia mjamzito aliyejifungua pacha na kusababisha kifo cha mtoto mmoja.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Ramadhan Ng’anzi alisema tukio hilo lilitokea Mei 15.

“Tunamshikilia kwa makosa matatu, likiwamo la uzembe, kufanya makusudi na kushindwa kuwajibika sawa na kiapo cha kazi yake, tunaendelea na mahojiano yatakapokamilika atafikishwa mahakamani,” alisema Ng’anzi.

Akisimulia chanzo cha mwanae kupoteza maisha, Shida Mugesi akiwa katika Hospitali ya Nyerere alisema alifika zahanati saa 12 asubuhi na kumuomba mganga amuhudumie, lakini alikataa.

“Nilikaa kwa muda wa saa mbili bila kupatiwa huduma, ghafla nilihisi uchungu wa kusukuma mtoto tukamuita mganga wa zamu ili anisaidie aligoma na kudai nimsubiri anakwenda kuoga na wakati huo alikuwa anazungumza kwa simu bila kuonyesha ushirikiano. Nilianza kujifungua mwenyewe,” alisema.

Muuguzi ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema walipopima uzito wa watoto kwa mjamzito huyo walibaini kuwa aliyefariki alikuwa na kilo 2.5 na mwingine 2.3.

Muuguzi wa zahanati hiyo, Frida Kasonga alisema aliposikia taarifa ya kuwapo kwa mgonjwa huyo alilazimika kurudi kituoni kumsaidia lakini alikuta mtoto mmoja ameshafariki dunia.

“Haikuwa zamu yangu ila nililazimika kurudi baada ya kusikia mganga aliyekuwa zamu kagoma kuwasaidia,” alisema Frida.

Ofisa mtendaji kata, Fadhila Nyamburapi na Mwenyekiti wa kitogoji cha Kazi, Samwel Nyakande walilaani kitendo hicho na kutaka sheria ichukue mkondo wake.

No comments:

Post a Comment