WAHITIMU
sita wa mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), wamepandishwa katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka matatu ikiwemo
kufanya mkusanyiko usio halali na kushawishi wenzao kuandamana kwenda
Ikulu kudai ajira, anaandika Faki Sosi.
Washtakiwa
katika kesi hiyo ni George Mgoba, mwenyekiti wao; Parali Kiwango,
makamu mwenyekiti; Linus Steven, katibu wa umoja wa wahitimu hao na
wahitimu wengine, Emmanuel Mwasyembe, Ridhiwani Ngowi na Jacob
Mang’wita.
Akiwasomea
mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi, Respicius Mwijage, Wakili
Mwandamizi wa Serikali, Benard Kongola amesema, washitakiwa hao
wanadaiwa kwamba 15 Februari 2014 katika eneo la Msimbazi Centre, Ilala
Dar es Salaam walipanga njama za kutenda makosa hayo.
Katika
shitaka lingine watuhumiwa hao wanadaiwa kufanya mkusanyiko usio halali
kwa lengo la kuandamana kwenda kwa Rais kulazimisha kupewa ajira katika
utumishi wa umma, jambo ambalo ni kinyume cha sheria na kwamba, hatua
hiyo ingesababisha uvunjifu wa amani.
Kwa
upande wa mshitakiwa Mgoba, Kiwango na Steven, wanadaiwa siku hiyo
katika eneo hilo, walishawishi wahitimu wenzao wa mafunzo ya JKT,
kufanya maandamano kwenda kwa Rais kulazimisha wapewe ajira katika
utumishi wa umma jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Washtakiwa
hao wamepandishwa kizimbani ikiwa ni siku chache baada ya kesi dhidi
yao kufutwa na kuachiwa Mei 26, mwaka huu kisha kukamatwa tena na leo
kupandishwa mahakamani kwa mashtaka hayohayo.
Katika
kesi ya awali iliyokuwa ikisikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi, Emilius
Mchauru, tayari mashahidi saba walikuwa wameshatoa ushahidi mahakamani
hapo huku akiwa amebakia shahidi mmoja tu ili kufunga ushahidi ndipo
kesi hiyo ilipofutwa na watuhumiwa hao kukamatwa tena na kusomewa
mashtaka hayo.
Watuhumiwa hao wamerudishwa rumande hadi kesi hiyo itakapotajwa tena Juni 9 Mwaka huu.
No comments:
Post a Comment