Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager leo imefanya mazoezi katika uwanja wa Omnisports Idriss Mahamat Ouya ulipo katika jiji la D’jamena ikiwa ni maandalizi ya mchezo dhidi ya wenyeji Chad siku ya Jumatano.
Taifa Stars imefanya mazoezi kuanzia majira ya saa 9 alasiri, ikiwa ni sawa na muda utakaochezwa mchezo siku ya Jumatano sawa na saa 11 kwa saa za nyumbani Tanzania na Afrika Mashariki.
Akiongelea maandalizi ya mchezo huo, Kocha Mkuu wa Taif Stars Charles Boniface Mkwasa amesema anashukuru vijana wake waliotangulia wamefika salama, hakuna majeruhi na wote wameweza kufanya mazoezi aliyoyapangilia.
“Hapa D’jamena hali ya hewa ni joto kali tofauti na nyumbani, kwa hizi siku mbili tutakazofanya mazoezi hapa, naimani vijana wataweza kuzoea hali ya hewa na kufanya vizuri katika mchezo wa Jumatano” alisema Mkwasa.
Mkwasa amesema wachezaji wake wametoka katika vilabu vyao ambavyo vilikua na michezo mwishoni mwa wiki, wote bado wako fit kikubwa wanafanya maandalizi ya mwisho kwa ajili ya mchezo huo.
“Hatujapata muda mrefu wa kufanya mazoezi kwa pamoja, wachezaji walikua na majukumu katika vilabu vyao, nashukuru wote wamewasili wakiwa salama na kesho wataungana na wachezaji wenzao wanaokuja katika kundi la pili kwa ajili ya mazoezi ya mwisho na mchezo wenyewe” aliongeza Mkwasa.
No comments:
Post a Comment