Spika wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai (Mb) amefanya mabadiliko ya baadhi
ya Wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge ili kuzingatia mahitaji mapya na
changamoto zilizojitokeza baada ya kuunda Kamati hizo mwezi Januari
2016.
Taarifa hiyo imetolewa leo Jijini
Dar es Salaam na Ofisi ya Bunge Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano
ambapo imeelezwa kuwa, mabadiliko hayo, yamefanywa chini ya Kanuni ya
116(3) ya Kanuni za Kudumu za Bunge inayompa Spika Mamlaka ya kuteua
Wabunge kuunda Kamati Mbalimbali za Bunge.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa,
kufuatia mabadiliko hayo ambayo baadhi yake yamehusu Mwenyekiti, Makamu
Mwenyekiti au wote wawili, Kamati za Kudumu za Bunge zilizoathirika na
mabadiliko haya zitawajibika kufanya Uchaguzi wa viongozi kwa mujibu wa
kanuni ya 116 (10).
Baadhi ya Kamati ambazo
zimeathirika na mabadiliko hayo na ambazo zitawajibika kufanya uchaguzi
kwa viongozi ni zikiwemo; Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii ambayo
itahitaji kupata Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wapya, Kamati ya
Nishati na Madini ambayo itahitaji kupata Mwenyekiti mpya, Kamati ya
Uwekezaji wa Mitaji ya Umma itahitaji kupata Mwenyekiti mpya, Kamati ya
LAAC ambayo pia itahitaji kupata Makamu Mwenyekiti mpya na Kamati ya
Huduma na Maendeleo ya Jamii ambayo itahitaji kupata Makamu Mwenyekiti
mpya.
Aidha, taarifa hiyo imeeleza pia
mabadiliko hayo kwenye kamati zote yanaanza mara moja ambapo orodha ya
wajumbe waliobadilishwa imeshatolewa na Ofisi hiyo na kusambazwa katika
vyombo vya habari.
No comments:
Post a Comment