SERIKALI
imeanzisha mfumo wa Kielektroniki wa malipo ya mishahara kwa watumishi
wa umma ambao unalenga kuondoa tatizo la madai ya malimbikizo ya stahili
zao.
Hayo
yamesemwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa jana (Jumamosi, Machi 5, 2016)
wakati akizungumza na watumishi wa sekta mbalimbali katika wilaya ya
Meatu, mkoani Simiyu.
Waziri
Mkuu alisema mfumo huo ujulikanao kama LAWSON, unatumika kwenye ajira
za watumishi wote nchini, wa Serikali Kuu na wale wa Serikali za Mitaa
Waziri
Mkuu alisema mfumo huo unasaidia kutunza, kutuma na kuhuisha taarifa
za watumishi kwa wakati na kwa ufanisi tangu mtu anapoajiriwa hadi
inapofikia wakati wa kupandishwa madaraja na hadi anapostaafu.
Kabla
ya kuanzishwa kwa mfumo huo, maafisa utumishi walipaswa kukusanya
taarifa za watumishi wote walioajiriwa na kuzipeleka Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma ili zikathibitishwe kabla ya kuzipeleka
HAZINA kwa maandalizi ya mishahara.
Akitolea
mfano wa kada ya ualimu, Waziri Mkuu alisema ajira za walimu zilikuwa
zinaanzia Idara ya Utumishi wa Walimu (TSD) lakini anapaswa aende
kuripoti kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri (DED) ambaye ni mwajiri
wake chini ya TAMISEMI.
"Hii ilileta ugumu wa malipo ya kupanda madaraja, uhamisho ama likizo kwa sababu mwajiri anakuwa hajatenga hizo fedha."
"Sasa
hivi tuna Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) ambayo iko chini ya
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri. Kwa hiyo ni rahisi wao kukaa pamoja
na kuamua tuwapandishe daraja walimu 10 na wote hao wakalipwa bila bila
kuchelewa," alisema.
Alisema
mfumo huo umeanza kutumika tangu mwaka 2012 na ulianza kwa ajira mpya
za walimu na hadi sasa umethibitisha kuwa inawezekana kumlipa mtumishi
mshahara wake hata kama ameajiriwa ndani ya mwezi huohuo.
"Kama
mtumishi anaripoti kwenye kituo kipya hata iwe wilaya ya wapi ili mradi
amefika na barua zake zote na ziko sahihi mtu huyu ataingiziwa taarifa
zake na wakati huohuo taarifa zitaonekana Ofisi ya Rais Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na pia zitapokelewa kwa maafisa wanaoshughikia
mishahara kule HAZINA."
Alisema
changamoto pekee waliyokutana nayo wakati mfumo huo umeanza ilikuwa ni
kutoingizwa taarifa za wale ambao wameripoti baada ya tarehe 10 ya mwezi
husika.
"Hii
ni kwa sababu matayarisho ya mishahara yanakuwa yameshaanza. Kwa hiyo
wengi walishauriwa kuripoti kati ya tarehe 25 hadi tarehe 9 ya mwezi
uliofuata na wote hawa hawakupata matatizo ya kucheleweshewa mshahara," alisema.
Akifafanua
kuhusu upandishaji madaraja ya watumishi, Waziri Mkuu alisema Serikali
imeondoa utaratibu wa mtumishi kulazimika kuandika barua ya kukiri
kupandishwa daraja/cheo ndipo aanze kupata stahili zake mpya.
"Hii
imeondoa ucheleweshaji wa kufanyika marekebisho ya mshahara na pili
imeondoa tofauti za mishahara kwa watumishi wenye ngazi moja (sifa sawa
za kitaaluma, tarehe moja ya kuajiriwa) ambao walikuwa wakilipwa tofauti
kwa sababu mmoja aliwahi kuandika barua ya kukiri na mwingine
alichelewa kuandika barua hiyo hiyo " alisema
AKATISHA ZIARA KUTOKANA NA MSIBA
Wakati
huohuo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amelazimika kukatisha ziara ya mkoa
wa Simiyu ambayo ilikuwa imalizike kesho kutokana na msiba wa
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa ambayo alipangiwa
kuitembelea leo.
Mkurugenzi
huyo Bw. Traceas Kagenzi alifariki dunia usiku wa kuamkia jana kutokana
na shinikizo la damu. Atasafirishwa kwenda Muleba kwa mazishi.
Akitoa
salamu za rambirambi kwenye ibada ya kumuombea marehemu Kagenzi
iliyofanyika nyumbani kwake Maswa mjini, Waziri Mkuu alisema ameshtushwa
na msiba huo uliotokea ghafla na kwamba Taifa limempoteza mtumishi
mahiri ambaye bado Taifa lilikuwa likimtegemea.
"Nimeshtushwa
sana na taarifa za msiba huu. Nimeambiwa hadi juzi usiku alikuwa
akishirikiana na Mkuu wa Wilaya hii kuandika taarifa ya ziara ya wilaya
hii. Kwa niaba ya Serikali, ninawapa pole sana wafiwa na Mungu awape
uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi," alisema.
"Nimelazimika kukatisha ziara ya mkoa huu kwa sababu huyu ni mtumishi mwenzetu" alisema Waziri Mkuu.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, MACHI 6, 2016.
No comments:
Post a Comment