Madereva watatu wa malori yaendayo mikoani na wasaidizi wao watatu,
wamenusurika kifo baada ya kupigwa risasi sehemu mbalimbali za mwilini
na mlinzi wa nyumba moja ya wageni iliyopo Ubena, Chalinze mkoani Pwani.
Tukio hilo limetokea jana alfajiri saa 11.30 kwenye hoteli hiyo
ambako madereva na wasaidizi hao walikuwa wamefikia kwa mapumziko kabla
ya kuendelea na safari.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Boniventura
Mushongi alisema tukio hilo lilitokea baada ya kuwapo kutokuelewana kati
ya mmoja wa madereva na mlinzi wa nyumba hiyo.
Kamanda Mushongi
alisema taarifa za awali zinasema baada ya mabishano hayo ambayo bado
hayajajulikana chanzo chake, mlinzi huyo alikoki silaha yake aina ya
Shortgun na kupiga risasi moja hewani kutuliza vurugu na kumjeruhi mmoja
wa madereva hao.
Hata hivyo, mabishano yalizidi baada ya
madereva wengine kujitokeza kuingilia ndipo mlinzi huyo akapiga risasi
nyingine ambayo ilitoka na gololi zake kusambaa na kuwajeruhi wengine
wanne ambao walipelekwa Kituo cha Afya Chalinze kwa matibabu.
Alisema mlinzi huyo amekimbia na anaendelea kutafutwa na chanzo cha tukio hilo kinachunguzwa.
Mganga
Mkuu wa Hospitali ya Chalinze, Dk Victor Bamba alisema walipokea
majeruhi watano ambao walipatiwa huduma ya kwanza na kutokana na hali
zao kuwa mbaya walihamishiwa Hospitali ya Tumbi.
Akizungumza
wodini Tumbi walikolazwa, mmoja wa madereva hao, Harun Adeli alisema
walifika hapo juzi saa mbili usiku na kuamua kulala ndani ya magari yao
ili jana waendelee na safari na ilipofika saa kumi na moja alfajiri
walisikia makelele yanayoashiria ugomvi ndani ya hoteli hiyo.
“Wakati tunashangaa tulishtukia risasi zinarindima na ndipo zilipotufikia,” alisema.
Muuguzi
wa zamu katika Hospitali ya Tumbi, Habibu Yahaya alisema aliwapokea
majeruhi Stephen Fredy, Beno Henry, Akrey Dallu, Ramadhani Saidi, Amani
Almasi na Adel wote wakazi wa Dar es Salaam.
Diwani wa Ubena,
Nicolaus Muyunga alisema kwa mujibu wa majirani, yalitokea mabishano
kati ya utingo na dereva ambao walikuwa wamekunywa na kulala kwenye meza
muda mrefu, walipotakiwa kuchukua vyumba wakalale ndani au warudi
katika magari yao walikataa na mlinzi alipotaka kuwaondoa kwa nguvu
walimzidi nguvu, hivyo akajitetea kwa kupiga risasi hewani.
No comments:
Post a Comment