Wednesday, 13 January 2016

Pato la Taifa laendelea kukua


Pato la Taifa katika kipindi cha Robo tatu ya mwaka 2015 limeendelea kukua kwa kasi ya asilimia 6.3 ikilinganishwa na kasi ya asilimia 5.4 katika kipindi cha mwaka 2014.
 
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa alipokuwa akiongea na waandishi wa Habari leo jijini Dar es Salaam.
 
Dkt. Albina amesema kuwa kutokana na ongezeko hilo Serikali imeendelea kutoa huduma za kijamii zikiwemo umeme, afya na maji.
 
“ Pato la Taifa kwa robo tatu ya mwaka 2015 limeendelea kukua kwa kasi ya asilimia 6.3 ukilinganisha na asilimia 5.4 katika robo tatu ya mwaka 2014” Alisema Dkt. Albina.
 
Dkt. Albina ameongeza kuwa kuongezeka kwa Pato la Taifa kumeenda sanjari na kuongezeka kwa thamani ya bidhaa na huduma nje ya nchi kwa takribani asilimia 3.3 ambapo bidhaa na huduma zilizochangia ongezeko hilo ni pamoja na dhahabu, Almasi, madini mengine na Utalii.
 
Aliongeza kuwa utangazwaji wa Takwimu za Pato la Taifa unazingatia matakwa ya Sheria ya Takwimu na 9 ya mwaka 2015 inayotoa mamlaka kwa Tume ya Taifa ya Takwimu kukusanya, kuchambua na kutangaza takwimu za Pato la Taifa.
 
Aidha alitaja baadhi ya shughuli za kiuchumi zilizokua kwa kasi kubwa katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2015 kuwa ni pamoja na Ujenzi (17.6%), Uchukuzi na Uhifadhi (10.6%), Uendeshaji Serikali na Ulinzi (10.6%) na Uchimbaji Madini na Kokoto (8.0%)
 
Dkt. Albina amesema kuwa jumla ya thamani ya Pato la Taifa kwa bei za miaka husika katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Septemba 2015 ni takribani shilingi tilioni 71.7 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 6.9.

No comments:

Post a Comment