Saturday, 2 January 2016

Makatibu wakuu wala kiapo cha maadili hadharani

Walioapa kiapo hicho ni makatibu wakuu 29 na manaibu katibu wakuu 21 huku wakielezwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue kuwa leo saa nne asubuhi, wanatakiwa kufika kufanyiwa semina elekezi. Makatibu hao walikula kiapo hicho, baada ya makatibu wakuu 12 na manaibu 14 wapya, kuapa kisha wote kwa pamoja kusaini kiapo hicho cha maadili, wakiongozwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Sefue.
Awali baada ya Kamishna wa Maadili, Waziri Kipacha kusoma tamko la kiapo hicho cha maadili, Rais John Magufuli aliingilia kati na kuwaomba makatibu hao wakuu kuwa kama yupo ambaye hajaridhishwa na maelezo hayo, akae pembeni kwani wasije wakawa wanazungumza tu, kumbe si wote wanaokubaliana.
Katibu Mkuu Kiongozi alisema kitendo hicho cha kula kiapo ni maalumu kwa lengo la serikali kukabiliana na tatizo la ukosefu wa maadili kwa watendaji wake, hali ambayo imekuwa ikisababisha wananchi kulalamika.
Alisema kabla ya kusaini kiapo hicho, makatibu wakuu na manaibu wasome kwa pamoja na kwa sauti kisha mmoja mmoja kusaini, kama ishara ya kukubali kufanya kazi kwa mujibu wa kiapo hicho, ambapo atakayeenda kinyume, yuko tayari kuchukuliwa hatua stahili.
Kamishna wa Maadili alisoma kiapo hicho cha maadili, kilichoeleza kuzingatia misingi ya maadili katika katiba na masharti ya sheria na ya maadili kwa viongozi wa umma kukuza utu, uwazi, uadilifu na uwajibikaji na kuimarisha imani kwa serikali kwa kuwa mzalendo na mwadilifu katika mpango wa utumishi wa umma.
Kiapo hicho pia kinaeleza kutotumia cheo au wadhifa kwa maslahi binafsi, familia au ndugu, bali kwa maslahi ya umma na kutekeleza majukumu kwa kufuata sheria, miongozo na taratibu za utumishi wa umma.
Vile vile kiapo hicho kinaeleza kutoomba, kushawishi, kutoa au kupokea rushwa au kupokea zawadi zozote kwa sababu za kiuchumi, kisiasa au kijamii zisizoruhusiwa kisheria na kutotoa shinikizo katika ajira, kupandishwa cheo au mikataba yoyote kutokana na cheo.
Kiapo kinawataka pia kutotoa siri za serikali au wateja kwa watu wasiohusika, bali kwa maslahi ya umma na kufanya uamuzi kwa maslahi ya umma na kutoa huduma bila upendeleo na kuepuka ukiukwaji wa sheria ya utumishi wa umma hata nje ya mahali pa kazi.
Katika tamko hilo, pia wanakiri kusoma na kusema wasipotekeleza masharti hayo na sheria nyingine zinaowaongoza za nchi, hatua za kisheria zinaweza kuchukuliwa dhidi yao, hivyo kiapo hicho kuwa ushahidi tosha. Baada ya kusainiwa na kamishna wa maadili, nakala moja walipewa kwa ajili ya kumbukumbu yao.
Katibu Mkuu Kiongozi Sefue alirudia kuwasihi makatibu, kama wote wamekubaliana na kiapo na kisha aliwataka kusimama na kunyanyua mkono kwa kulia kwa ajili ya kuapa ; huku akiwaeleza na kuwasisitiza kuhakikisha wafike leo asubuhi kwa ajili ya semina elekezi.
Kauli ya Waziri Mkuu Mara baada ya kiapo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwapongeza viongozi hao na kuwataka kuwa waaminifu, kuwajibika na kutoa taarifa za utendaji kwa wananchi.
Majaliwa alieleza kuwa sasa serikali imeamua kudhibiti utendaji kazi kuwa wa uwazi, uadilifu, uaminifu, utendaji unaoweza kutoa matokeo tarajiwa kwa wananchi ambao ni walengwa wakuu wa serikali.
Alisema utaratibu huo utaendelea kwa wakuu wa mikoa , wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri za wilaya wote na kwamba watakaoteuliwa wataapa mbele ya kamishna wa maadili, kuwaeleza Watanzania kuwa wamepewa jukumu la kuwatumikia wananchi.
“Jukumu hilo ni kwenda sambamba na kusimamia utekelezaji wa miradi na usimamizi wa fedha kwa kusimamia matumizi kwa ajili ya miradi ya wananchi, kwa wakuu wa wilaya kama wasimamizi wa serikali watahakikisha fedha zilizoenda katika halmashauri na wilaya zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa,” alisema.
Alisema fomu hiyo ni tamko rasmi, ambalo linambana mhusika kwa kuwa ameridhia, hivyo kama Rais alivyoonesha nia ya utendaji kazi serikali, Watanzania waendelee kuwa na imani na utendaji kazi wa serikali, katika kusimamia maeneo yote na yale ambayo Rais na Makamu wake waliahidi wakati wa kampeni yanafanyiwa kazi.
Ahadi za makatibu wakuu Makatibu wakuu hao walieleza nia yao ya kushirikiana na serikali, kukomesha matatizo mbalimbali, kusimamia Sheria, kulinda maslahi ya Watanzania na kusimamia falsafa ya ‘Hapa Kazi Tu.’ Makatibu hao ambao ni watendaji wakuu katika wizara, walisema hayo katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es Salaam jana.
Waliahidi kufanya kazi kwa lengo la kuwatumikia wananchi na kwamba hawatamwangusha Rais Magufuli. Katibu Mkuu mpya wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi alisema amedhamiria kuhakikisha anatokomeza tatizo la ujangili nchini.
Alisema changamoto kubwa inayoikabili wizara hiyo ni ujangili na kuahidi ataifanyia kazi mapema, kwani ni aibu kwa nchi kuendelea kupoteza wanyama, hivyo na kuikosesha nchi pato kubwa la nchi linatokana na utalii unaotegemea wanyama.
“Rais amesisitiza suala la ujangili, kwani siyo vizuri na siyo sahihi nchi kuendela kukosa wanyama kutokana na watu wenye uchu na uchoyo na ubinafsi kwani ni changamoto kubwa licha ya wizara kuanza kuchukua hatua kwa kuangalia walipofikia,” alisema.
Aliahidi kuangalia changamoto nyingine atakapofika ofisini, lakini hilo la ujangili atalishughulikia moja kwa moja na matatizo ya vitalu na migogoro ya maeneo kati ya hifadhi na wananchi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Meja Jenerali Projest Rwegasira alisema ni mapema mno kuzungumzia masuala ya wizara hiyo, kwani ana jukumu katika kusimamia usalama wa raia.
Alisema amejipanga vizuri kufanya kazi kwa uadilifu na uaminifu katika nafasi hiyo, ambayo rais amemuamini na kumpatia. Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria , Amon Mpanju ambaye ni Mwenyekiti wa shirikisho la walemavu nchini, akiwa na ulemavu wa kutoona ambaye alishangiliwa sana wakati wa kuapishwa, aliahidi kuwathibitishia kuwa ulemavu alionao, hauhusiani na akili.
Alisema hali aliyonayo haikumzuia kuwa mwanasheria, hivyo ana uwezo wa kufanya kazi inavyotakiwa. Alimshukuru Rais kwa kuamini watu wenye ulemavu na kuwaweka katika nafasi za utendaji.
Mpanju alisema Rais Magufuli ameandika historia mpya nchini kwa kuwaweka walemavu kuongoza katika utendaji. Aliahidi kutumia uwezo wake na taaluma aliyonayo kuwatumikia watanzania vyema.
“Katika wizara nitahakikisha sheria zinarekebishwa kulinda maslahi ya watanzania wote kwa kuwa na mifumo mizuri ya sheria, ikiwemo suala la katiba huku walemavu nao akiwaangalia kwa kuwa na sheria zitakazokuwa na maslahi kwao,” alisisitiza.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Dk Juliana Pallangyo alisema atafanya kazi kwa ushirikiano wa viongozi wa serikali kwa kufuata maelekezo na sera, kuhakikisha wananchi wananufaika na umeme na madini.
Alisema wizara itahakikisha kunakuwa na umeme wa kutosha, hasa baada ya kuwa na gesi ya kutosha na vyanzo vingine, jambo litasaidia wananchi kuacha kulalamikia suala la umeme.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Ngosi Mwihava alisema katika wizara hiyo wanashughulikia Mazingira na Muungano, hivyo atahakikisha Muungano unaimarika na kukabili changamoto zilizopo.
Alisema kwa sasa kipaumbele chake ni kuhakikisha Zanzibar inafanya Uchaguzi Mkuu wa kuchagua Rais baada ya kuahirishwa kwa amani na maridhiano kwa kushirikiana na kamati ya maridhiano inayoendelea na kazi.
Akizungumzia mazingira alisema watahakikisha kila mtu anapunguza uharibifu wa mazingira kwa lengo la kudhibiti athari zake hapo baadaye kwa kila mmoja kuona ni jukumu lake.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Moses Kusiluka alisema atafanya kazi zake kwa uadilifu na kusimamia utekelezaji wa sheria pamoja na kuendeleza miji.

No comments:

Post a Comment