Alisema, kazi ya kutumbua majipu ni kubwa, lakini Watanzania hawana budi kushirikiana kwa pamoja ili kutimiza azma ya kupambana na ubadhirifu pamoja na ufisadi wote. “Maombi haya kwa ajili ya taifa letu ni muhimu sana, muendelee kuliombea taifa na viongozi wake ili waweze kutekeleza dhamira ya kuleta maendeleo katika nchi...viongozi wa dini muendelee kuisihi jamii kuishi kwa kufuata maadili mema,” alisema.
“Maombi yatasaidia jamii kuachana na vitendo vya rushwa, ufisadi, matumizi ya dawa za kulevya pamoja na mambo mengine yaliyo kinyume na maadili, mambo haya yanapaswa kufanyiwa maombi maalumu,” alisema Rais.
Alisema serikali inatambua kuwa wapo watendaji ambao si waaminifu, wanaoshiriki kuiba dawa hospitalini, hawafanyi kazi zao ipasavyo, wanaoiba fedha za umma, wanapokea na kutoa rushwa na wanaosababisha upotevu wa mapato ya serikali, lakini peke yake bila ushirikiano wa wananchi hataweza kumaliza matatizo hayo, pia viongozi wa dini kukemea mambo hayo kwa kuwa watu hao ni waumini wa dini mbalimbali.
Aliwataka viongozi wa madhehebu yote ya dini, kusisitiza waumini wao kufanya kazi kwa bidii, kwani hata vitabu vitakatifu vya Biblia na Quran, vinasisitiza watu kufanya kazi kwa bidii. Alisema Mwenyezi Mungu amewachagua viongozi wa dini, kuwaongoza waumini katika njia nzuri, hivyo mafundisho yao watu wanayapokea katika namna ya pekee; na kwamba hawana budi kukemea mambo ambayo yanarudisha nyuma maendeleo.
Aidha, aliwataka kuhakikisha wanahimiza waumini wao kuendelea kupendana, kuwa wamoja na kudumisha amani iliyopo, ambayo imedumu kwa muda mrefu na kwamba Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kusimamia misingi iliyoasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Rais Magufuli alisema serikali itaendelea kuhakikisha hakuna ubaguzi wa aina yoyote, utakaofanyika baina ya Watanzania wenyewe, kwani ni jambo ambalo Mwalimu Nyerere alilikemea tangu zamani, pia kila Mtanzania kuwa na uhuru wa kuabudu dini aitakayo bila kuvunja sheria za nchi.
“Serikali itaendelea kutoa fursa sawa za kiuchumi ili kila mmoja aweze kunufaika na taifa letu liweze kusonga mbele katika kujiletea maendeleo...mkesha huu ni muhimu kwa mustakabali wa taifa letu, dua na sala zenu ni muhimu katika kumaliza maovu yanayotendeka,” alisema.
Aliomba Watanzania kuendelea kumuombea ili aweze kutenda kazi yake na kutimiza ahadi zake za kuwatumikia na kuwaletea maendeleo wananchi.
Waziri wa Habari, Michezo, Utamaduni na Sanaa, Nape Nnauye alisema ni jambo la kumshukuru Mungu kwa kuvuka salama katika uchaguzi mkuu, kwani salama hiyo haitokani na akili za wanasiasa, bali Mungu mwenyewe ndiyo ameamua.
Alisema pia ni jambo zuri kumshukuru Mungu kwa kumpata Rais mzuri, ambaye amekuwa gumzo dunia nzima na hata baadhi ya wananchi wa nchi jirani, wakiomba kumpata rais kama huyo; na wengine wakiomba waazimwe akawe rais wao kwa muda.
“Tuendelee kumuomba Mungu, ampe nguvu ya kutumbua majipu ili nchi yetu iweze kusonga mbele kimaendeleo,” alisema Nape. Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mkesha huo, Askofu Godfrey Malassy alisema lengo la mkesho huo ni kumshukuru Mungu kwa kuiwezesha Tanzania kuvuka salama katika uchaguzi mkuu, licha ya kuwepo kwa viashiria vya vurugu na pia kuliombea taifa pamoja na Rais Magufuli.
Alisema kulikuwa na hatari ya kuvunjika kwa umoja wa Watanzania, lakini Mungu aliweza kusimamia hadi sasa wote ni wamoja, licha ya kuwepo kwa maneno mabaya ya watu wasiotakia mema Tanzania.
“Mkesha huu pia ni kwa ajili ya kufanya dua ya kuliombea taifa letu kuwa na maendeleo endelevu na Rais wetu Magufuli aweze kutekeleza majukumu yake... kasi yake imeonekana na kila Mtanzania amefurahishwa nayo,” alisema.
Alisema sadaka zilizopatikana katika mkesha huo, zitaenda kusaidia katika sekta ya afya kwa kuweka huduma ya umeme jua katika hospitali mbalimbali mkoani Tabora, kutokana na akinamama wengi wajawazito kujifungua kwa shida gizani na hata wakati mwingine watoto kufa kutokana na kukosekana kwa nishati hiyo. Aliongeza viongozi wa dini, wataendelea kuwa nae bega kwa bega ili atimize dhamira ya kuwaletea maendeleo wananchi.
No comments:
Post a Comment