Seif Sharif Hamad, |
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharif Hamad, amemwangukia Papa
Francis kwa kumwandikia barua, akimuomba kutumia ushawishi wake na
Tanzania kumaliza mzozo wa kisiasa kisiwani humo kabla hali haijawa
mbaya.
Kwa
mujibu wa barua yake ya Novemba 25, mwaka jana, Maalim Seif alimwomba
Papa kutumia ushawishi alionao kwa serikali ya Tanzania ili kuhakikisha
haki inatendeka na kuepusha vurugu zinazoweza kutokea.
“Ni
wiki tatu sasa tangu kufanyika kwa uchaguzi mkuu na hali hii
imesababisha kusimama kwa baadhi ya shughuli za kuichumi kutokana na
wananchi wengi kuwa na hofu kuhusu mustakabali wa hali hii….watu
wanashindwa kujua nini kitatokea maana wana hofu kwamba hali hii inaweza
kuharibu umoja wa kitaifa kwa watu kuishi kwa upendo bila kujali dini
wala kabila,” ilisema barua hiyo.
Barua
hiyo ya Maalim Seif ilisema, Zanzibar ina mchanganyiko wa Waislamu na
Wakristo, hivyo hakuna mgawanyiko kwa misingi ya udini lakini hatua ya
wananchi kukosa haki yao ya kidemokrasia kupitia sanduku la kura baada
ya miaka 20 ya chaguzi visiwani humo kunaweza kusababisha vijana ambao
hawafurahishwi na mwenendo huo kutumia njia mbaya kutafuta haki yao.
“Badala
ya kuchukua hatua za pamoja kuzuia uovu huu, Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ambayo chama chake kilishinda kwenye uchaguzi mkuu
uliopita, imekuwa ikisaidia serikali ya Zanzibar kwa kutumia askari na
majeshi yake kutishia watu wa upinzani,” ilisema.
“Wakati
mmishenari wa kikristu alipomuomba Sultan wa Zanzibar mwaka 1840
kibali cha kujenga asasi ya kusaidia jamii kwenye eneo lake, Sultani
yule ambaye alikuwa Muislamu alimtambua kama mtumishi wa Mungu aliyekuwa
na lengo la kuendeleza neno la Mungu” ilisema sehemu ya barua hiyo kwenda kwa Papa.
Iliongeza
kuwa, Zanzibar ilipopata Uhuru wake mwaka 1963, kwa kiwango kikubwa
watu wake waliishi kwa amani na ushirikiano baina ya watu wa madhehebu
yote ya Katoliki, Anglikana, Sunni, Shia na Hindu na hakukuwahi kuwa na
mgogoro wala hofu ya watu hao kuhitilafiana kwa misingi ya tofauti ya
dini.
Ilisema
Chama cha Wananchi CUF kimekuwa kikishinda chaguzi zote tangu
kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1995, lakini haijawahi kupewa
ushindi wake hata muhula mmoja.
No comments:
Post a Comment