CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeanza maandalizi ya kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 39 ya kuzaliwa kwake ambapo kilele kitakuwa mkoani Singida ifikapo Februari 6, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye, alisema maadhimisho ya mwaka huu, yatahusisha shughuli mbalimbali zilizolenga kuhamasisha utekelezaji wa maendeleo nchini.
Nape alisema uzinduzi wa maadhimisho hayo utafanyika Januari 31, mwaka huu mjini Unguja, Zanzibar na mgeni rasmi atakuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein.
Alisema kilele cha maadhimisho hayo ambayo mwaka huu kaulimbiu yake ni ‘Sasa kazi, kujenga nchi na kukijenga chama,’ kitafanyika mkoani Singida na mgeni rasmi atakuwa ni Rais mstaafu na Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Jakaya Kikwete.
“Viongozi wa kitaifa na baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu watakaohudhuria watapangiwa shughuli za ujenzi wa chama na taifa kwa ujumla katika wilaya zote za Mkoa wa Singida, siku tatu kabla ya kilele cha maadhimisho hayo,” alisisitiza Nape.
Aliitaka mikoa yote iandae shughuli maalumu kwa muda wa wiki nzima ya maadhimisho hayo, mkazo ukiwa ni kufanya shughuli za ujenzi wa chama hicho na taifa katika maeneo yao.
Aliyataja mambo ambayo mikoa yote inapaswa kuzingatia katika wiki hiyo ya maadhimisho kuwa ni kuingiza wanachama wapya wa chama hicho na jumuiya zake na kukiimarisha na kufanya mikutano ya kuwashukuru wana CCM na wananchi kwa kukiamini chama hicho kiendelee kuwaongoza.
Aidha, alisema mambo mengine ni kuhamasisha wananchi kufanya kazi ili kujiletea maendeleo yao binafsi na ya taifa na kushiriki shughuli za maendeleo ikiwemo ujenzi wa madarasa, zahanati, vituo vya afya, upandaji miti, uchimbaji wa mitaro ya maji, usafi wa mazingira na shughuli nyingine za kijamii.
Mwaka jana chama hicho, kiliadhimisha miaka 38 ya kuzaliwa kwake mkoani Ruvuma.
No comments:
Post a Comment