Thursday, 14 January 2016

Lowassa Amtembelea Sumaye Hospitalini.


Aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, amemtembelea Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, katika taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Hosptitali ya Taifa Muhimbili alikolazwa.

Lowassa ambaye alifika hospitalini hapo jana saa 7:00 mchana akiwa na mke wake Regina, aliwapongeza viongozi wengine ambao wamekwisha kufika hospitalini hapo kumjulia hali Sumaye, wakiwamo Rais John Magufuli, Rais Mstaafu na Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Lowassa alisema hilo ni jambo jema la  kiungwana, la kuheshimiana na kutendeana mema.

Wengine waliomtembelea Sumaye hospitalini hapo ni Waziri Mkuu Mstaafu, Dk. Salim Ahmed Salim na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema,  Prof. Mwesiga Baregu.

Lowassa na mkewe walifika hospitalini hapo muda mfupi baada ya Prof. Baregu na Dk. Salim kumuona Sumaye.

Akizungumza baada ya kutembelewa na hospitalini hapo, Sumaye alisema anaendelea vizuri.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa JKCI, Prof. Mohamed Janabi, alisema hali ya mgonjwa huyo imeendelea kuimarika kila siku.
 
Sumaye alilazwa katika taasisi hiyo siku sita zilizopita kwa matibabu ya moyo.

No comments:

Post a Comment