Simba
imeanza michuano ya Mapinduzi kwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Jamhuri ya
Pemba katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Amaan mjini Zanzibar.
Simba
ambao ni mabingwa watetezi wa kombe hilo walipanga kikosi cha wachezaji
wengi ambao wamekuwa hawapati nafasi ya kucheza katika mechi za Ligi Kuu
Bara na walionekana kutoelewana vizuri kabisa.
Pasi
nyingi kwa Simba hazikuweza kuisaidia ingawa ilianza kupata bao la
kwanza mapema tu kupitia kwa Awadhi Juma aliyelipa shuti kali nje ya 18,
hiyo ilikuwa ni dakika ya 12.
Lakini
Jamhuri wakasawazisha dakika chache baadaye kupitia kwa Mwalimu
Mohammed katika dakika ya 18 aliyefunga kutokana na safu ya ulinzi ya
Simba kuonekana kujichanganya huku Jonas Mkude na Mohammed Fakhi
wakionekana kutoelewana.
Jamhuri
ilipata bao la pili kupitia kwa Ammy Bangekesa katika dakika ya 52
mara tu baada ya kuanza kwa kipindi cha pili lililotokana na makosa
mengine ya Fakhi kabla ya Awadhi Juma kufunga bao la kusawazisha kwa
Simba katika dakika ya 76.
No comments:
Post a Comment