Monday, 11 January 2016

CUF: Uchaguzi unaweza kuzua vurugu Zanzibar

Seif


Chama cha Wananchi (CUF) kimeonya kuwa kurudiwa kwa uchaguzi visiwani Zanzibar kunaweza kusababisha vurugu na kumtaka Rais wa Tanzania Dkt John Magufuli kuingilia kazi kutatua mzozo ulitokana na uchaguzi visiwani humo.
Katibu mkuu wa chama hicho Maalim Seif, akihutubia wanahabari, amesema chama hicho hakitaki uchaguzi urudiwe na kuendelea kusisitiza msimamo wa awali kwamba mshindi wa uchaguzi uliofanywa 25 Oktoba mwaka jana anafaa kutangazwa.
"Ni vyema tukaweka waziwazi hapa kwamba kurudiwa uchaguzi sio suluhishona hakukubaliki. Kwani, kama nilivyoonesha hakuna hoja wala msingi wa kikatiba na kisheria wa uchaguzi kurudiwa," amesema Bw Seif.
Bw Maalim Seif, aliyekuwa mgombea urais wa chama hicho, alionekana kupendekeza mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jecha Salim Jecha ang’atuke.
Chama hicho kimemtuhumu Rais wa visiwani Mohamed Ali Shein wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kukwamisha mashauriano ya kutafuta suluhu ili ZEC itangaze marudio ya uchaguzi.
Ingawa tarehe kamili haijatangazwa, Bw Seif na wenzake wamedokeza kwamba huenda kukawa na mipango ya kuitisha marudi ya uchaguzi tarehe 28 Februari 2016.
CCM imeonekana kuunga mkono kurudiwa kwa uchaguzi visiwani na majuzi viongozi wa chama hicho waliwataka wafuasi wake visiwani kujiandaa kwa marudio ya uchaguzi.
Tangazo hilo lilishutumiwa vikali na viongozi wa CUF.

No comments:

Post a Comment