Wakazi wameambia BBC kwamba wapiganaji hao wa al-Shabab wamepandisha bendera yao katika kambi hiyo na kwamba walionyesha miili ya wanajeshi waliouawa katika barabara za mji huo.
Lakini msemaji wa majeshi ya Kenya Kanali David Obonyo amesema kambi iliyoshambuliwa si ya majeshi ya Kenya.
Badala yake, anasema kambi iliyo karibu ya wanajeshi wa Somalia ndiyo iliyovamiwa na majeshi ya Kenya yalijibu shambulio hilo.
Idadi ya waliofariki kutoka pande zote mbili bado haijabainika, Kanali Obonyo amesema kupitia taarifa.
Ameambia BBC kwamba ripoti kuwa wanajeshi wengi wameuawa ni “propaganda ya kawaida kutoka kwa al-Shabab”.
Kenya ina majeshi 4,000 kwenye kikosi cha AU nchini Somalia ambacho kina wanajeshi 22,000.
Kikosi hicho, ambacho hujulikana kama Amisom, huungwa mkono na Umoja wa Mataifa.
Mkazi wa el-Ade ameambia BBC kwa njia ya simu kwamba alisikia mlipuko mkubwa mwendo wa saa kumi na moja unusu alfajiri na baadaye akasikia ufyatuaji mkali wa risasi.
"Tuliona mpiganaji wa al-Shabab mjini. Na pia tuliwaona wanajeshi wa Kenya waliokuwa wanatoroka kambi.
"Kwa sasa kambi imo mikononi mwa al-Shabab. Tunaona magari ya kijeshi yakiteketea na maiti za wanajeshi zimetapakaa. Hakuna raia aliyeuawa lakini lakini watu wengi wameutoroka mji.”
“Tulichukua udhibiti wa kambi baada ya saa moja ya mapigano makali,” amesema.
“Tulihesabu miili 63 ya Wakenya ndani ya kambi hiyo. Wanajeshi hao wengine wa Kenya walitorokea msituni na tunawawinda.”
Alisema wapiganaji hao watachukua magari 28 ya kijeshi kati ya 31 yaliyokuwa kwenye kambi hiyo pamoja na silaha zote.
Kambi mbili za kijeshi, moja ya Majeshi ya Kitaifa ya Somalia (SNA) na nyingine ya AU, zinapatikana eneo moja viungani mwa mji wa el-Ade, ambao unapatikana katika jimbo la Gedo, kilomita 380 magharibi mwa mji wa Mogadishu.
Al-Shabab walifurushwa kutoka mji mkuu Mogadishu, Agosti 2011, lakini bado wana nguvu baadhi ya maeneo ya Somalia na hutekeleza mashambulio ya mara kwa mara nchini humo
No comments:
Post a Comment