Chama cha CUF
visiwani Zanzibar kimewataka wananchi visiwani humo kupuuza wito wa
chama tawala Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa kuwataka wazanzibari wajiandae
kwa marudio ya uchaguzi visiwani humo.
Mwandishi wa BBC Sammy Awami anasema kuwa CUF anasema kwamba
wito wa CCM juu ya maandalizi ya uchaguzi wakati bado vikao vya
usuruhishi wa mgogoro huo bado vinaendelea, ni kuwachanganya wananchi
juu ya nini hasa hatma ya mgogoro wa kisiasa visiwani humo Kwa muda wa zaidi ya mwezi mmoja sasa, viongozi wa
juu wa serikali na vyama, ikiwa ni pamoja na marais wastaafu wamekuwa
wakiendelea na vikao vya siri vinavyolenga kutafuta suluhu la mgogoro
huo wa kisiasa visiwani Zanzibar
Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo, Kaimu mkurugenzi wa habari na mawasiliano wa CUF Ismail Jussa amesema ''ni vema ikasubiriwa taarifa rasmi ya maafikiano ya vikao vinavyoendelea ambayo bado haijatolewa''
Tangu
kufutwa kwa uchaguzi visiwani Zanzibar, chama tawala CCM kiliunga mkono
kurudiwa kwa uchaguzi huku CUF ikiapa kuususia uchaguzi huo na kutaka
aliyekuwa mgombea urais wake Maalim Seif Sharif Hamad atangazwe kuwa
mshindi wa uchaguzi huo, ambao CUF inadai Maalim Seif alishinda kwa
asilimia zaidi ya 50%. Wanaohusika katika msururu wa vikao vya mashauriano
ya mgogoro wa Zanzibar ni pamoja na Rais wa Zanzibar Dokta Ali Mohamed
Shein, ambaye ndiye mwenyekiti huku wajumbe wakiwa ni makamu wa pili wa
rais balozi Seif Ali Iddi, marais wastaafu Amani Abeid Karume, Jakaya
Mrisho Kikwete, Ali Hassan Mwinyi, Dokta Salmin Amour Juma na makamu wa
kwanza wa rais Maalim Seif Sharrif Hamad ambaye ndiye mwakilishi kutoka
upande wa CUF.
Zanzibar iliingia katika mgogoro wa kisiasa miezi
miwili iliyopita baada ya mwenyekiti wa tume ya uchaguzi visiwani humo
Jecha Salim Jecha kufuta matokeo ya uchaguzi kwa kile alichokiita
ukiukwaji wa sheria na utaratibu wakati wa zoezi la upigaji kura.
No comments:
Post a Comment