VILIO vimetawala baada ya wakazi waishio katika eneo la Jangwani jijini Dar es Salaam kukumbwa na bomoabomoa ambapo nyumba zaidi ya 100 zimebomolewa katika siku ya kwanza katika eneo la Mkwajuni na Magomeni katika Manispaa ya Kinondoni.
Jana Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Manispaa za Jiji la Dar es Salaam, zilianza kazi ya kubomoa nyumba zote zilizo katika maeneo oevu, kando ya mito na bahari.
Mkuu wa Kitengo cha Sheria Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira Tanzania (NEMC), Manchale Heche alisema bomoabomoa hiyo inalenga kuzibomoa nyumba zaidi ya 4,000 zilizojengwa katika maeneo hayo huku nyingi zikiwa ni katika Bonde la mto Msimbazi.
“Leo hapa Jangwani tumeanza kwa kubomoa nyumba zaidi ya 100, lakini nyumba zaidi ya 4,000 zinatarajiwa kubomolewa na hizi ni zile zote ambazo zimejengwa katika maeneo ambayo yanakatazwa kisheria,” alisema Heche.
Heche alisema serikali ilishatoa tangazo la mwisho juu ya kuwataka wakazi wote waliojenga katika maeneo ya mabondeni, na maeneo yote hatarishi wahame, lakini watu wameendelea kukaidi.
“Tumekuwa tukiwasihi kuhama maeneo ya mabondeni kila mara, Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete ilishawatangazia wananchi wa mabondeni wahame na aliwapa viwanja huko Mabwepande, lakini wameviuza na kuendelea kujenga na kuishi mabondeni kinyume cha sheria za mazingira na mipango miji,” alifafanua Mwanasheria Heche.
Nyumba zitakazokumbwa na bomoabomoa hiyo ni zile zilizojengwa maeneo yote ya bondeni katika Bonde la Mto Msimbazi, kando ya mito na katika maeneo ya hifadhi ya bahari ndani ya mita 60.
Aidha, Mwanasheria huyo alisema bomoabomoa hiyo ni endelevu, hivyo kuwataka wananchi wote wanaoishi maeneo ya miundombinu na maeneo yote hatarishi, iki wemo katika fukwe za bahari, kingo za mito na mikondo ya bahari kuhamisha mali zao mapema kabla hawajafikiwa.
Wakazi wote waliopo katika Bonde la Mto Msimbazi, ikiwa ni kuanzia Jangwani hadi maeneo ya Gongo la Mboto, katika Manispaa ya Kinondoni, na kwingineko, wanapaswa kuhama.
Wakazi waliokutwa na kadhia hiyo, kwa nyakati tofauti wamesikika wakilalamika kutokuwa na taarifa japo mara kadhaa Rais mstaafu Jakaya Kikwete aliwatangazia kuhama kwa hiyari.
Heche alisema ubomoaji huo, haulengi Dar es Salaam pekee, bali ni kazi inayofanyika nchi nzima na wote waliojenga mabondeni na katika maeneo oevu, wahame.
Alisema wao wanalenga kulinda usalama wa wananchi kimazingira na kiafya kwa ujumla kwa maeneo hayo ni hatari na wenyewe ni mashuhuda pindi patokeapo mvua wanakumbwa na mafuriko.
Mwezi uliopita, Manispaa ya Kinondoni iliendesha bomoabomoa kwa watu waliojenga katika maeneo ya wazi na ilieleza kuwa kazi hiyo itakuwa endelevu
No comments:
Post a Comment