Thursday, 17 December 2015

ACT Wazalendo yatoa Meya Kigoma Ujiji

kiongozi wa chama cha ACT wazalendo zitto kabweakihutubia mkutano wa hadhara
 BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji limemchagua Diwani wa Kata ya Bangwe, Hussien Ruhavi kuwa Meya wa manispaa hiyo. Sambamba na hilo, Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini Zitto Kabwe (ACT Wazalendo) akiahidi kumshughulikia diwani yeyote atakayekwamisha mipango yao ya kuleta maendeleo katika manispaa hiyo.

Katika uchaguzi huo ambao Zitto alikuwa Mwenyekiti wa uchaguzi alimtangaza Ruhavi kutoka chama cha ACT Wazalendo kuwa mshindi kwa kupata kura 19 kati ya kura 21 zilizopigwa akimshinda mpinza wake Masudi Kassim (CCM) ambaye hakupata kura hata moja huku madiwani watano wa CCM wakigoma kupiga kura katika baraza hilo lenye madiwani 27.

Aidha Zitto alimtangaza diwani wa kata ya Buzebazeba, Athuman Mussa kupitia chama cha ACT Wazalendo kuwa Naibu Meya wa Manispaa ya Kigoma Ujiji akimshinda Mussa Maulid wa CCM aliyepata kura moja.
Baada ya kutangaza matokeo, Zitto alisema licha ya tangu awali kuonekana kwamba wagombea wa ACT ndiyo wangekuwa washindi katika uchaguzi wa viongozi wa manipaa hiyo, baadhi ya madiwani kwa makusudi waliamua ama kugoma kushiriki kwenye mchakato au kuharibu kura jambo ambalo linaonesha dhahiri kwamba madiwani hao hawako tayari kushirikiana na walio wengi. 

Kutokana na hilo, Mbunge huyo wa Jimbo la Kigoma Mjini alisema watasimamia mipango ya kuwaletea wananchi maendeleo kwa usawa. Alionya diwani ambaye kwa makusudi ataamua kukwamisha michakato mbalimbali ya maendeleo watamshughulikia kwa namna watanavyojua wao.

Akizungumza baada ya uchaguzi huo Meya wa manispaa ya Kigoma Ujiji, Hussein Ruhavi amewashukuru madiwani kwa imani kubwa aliyoonesha kwake na kumchagua kuwa meya wa manispaa hiyo.
Hata hivyo Ruhavi alisema atafaya kazi na kushirikiana na madiwani wote kwa ajili ya maendeleo ya wananchi na kuwataka madiwani wenzake kufanya kazi pamoja bila kujali itikadi za vyama vyao.
CHANZO; HABARI LEO

No comments:

Post a Comment