RAIS John Magufuli amekutana na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mgombea Urais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad katika Ikulu ya Dar es Salaam na kujadili hali ya kisiasa ya Zanzibar.
Kwa mujibu wa Ikulu, wawili hao wamekutana kutokana na maombi ya siku nyingi ya Maalim Seif, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF). Ikulu ilieleza kuwa mazungumzo ya viongozi hao, pia yalihudhuriwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
“Viongozi hawa kwa pamoja wamejadili hali ya kisiasa Zanzibar na wamefurahishwa na hali ya usalama na utulivu inayoendelea,” ilisema taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu jana.
“Aidha, Mheshimiwa Rais Magufuli amewapongeza Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Dk Ali Mohamed Shein, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad, na viongozi wote wanaoshiriki katika mazungumzo ya kuleta hali ya uelewano Zanzibar,” ilifafanua.
Rais Magufuli pia aliwapongeza na kuwashukuru wananchi wa Zanzibar kwa kudumisha amani na utulivu wakati wa mazungumzo baina ya viongozi wa CUF na CCM yakiendelea huko Zanzibar.
Katika mazungumzo hayo, Maalim Seif alimueleza Dk Magufuli juu ya hali ya siasa Zanzibar kadili anavyoielewa yeye ;na Rais Magufuli alimshukuru Makamu huyo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kwa taarifa yake nzuri, huku akimsihi waendelee na mazungumzo hadi suluhisho muafaka lipatikane.
Ikulu ilisema majadiliano yanayoendelea, yanatoa fursa ya kudumishwa kwa utulivu na sifa njema ya nchi, hivyo viongozi hao kwa pamoja wamewaomba wananchi waendelee kuwa watulivu ili kutoa nafasi ya majadiliano yanayoendelea kufikia hatma njema.
“Wameelezea matumaini yao kuwa vyama vya CCM na CUF haviwezi kushindwa kupata suluhu ya mgogoro huo,” iliongeza taarifa ya Ikulu na kuongeza: “Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amemuhakikishia kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano itahakikisha kuwa amani na utulivu unaendelea kudumishwa Zanzibar” Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa Oktoba 25, mwaka huu ulifutwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kutokana na kasoro zilizobainika.
No comments:
Post a Comment