Monday, 21 December 2015

KAGAME AMSIFIA MAGUFULI KWA UTUMBUAJI MAJIPU BANDALINI


Image result for kagame

 RAIS Paul Kagame wa Rwanda amefurahishwa na hatua ambazo Rais John Magufuli anazichukua, hasa katika usimamizi na utendaji kazi wa bandari huku akimhakikishia kuwa Rwanda iko tayari kushirikiana na Tanzania, hasa katika kuitumia Bandari ya Dar es Salaam.

Siku chache baada ya kuingia madarakani, Rais Magufuli akimtumia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alifanya ziara ya ghafla katika Bandari ya Dar es Salaam, ambako alifichua ufisadi wa mabilioni ya shilingi kutokana na upotevu wa makontena, ambayuo hayakulipiwa kodi stahili kwa serikali.

Kutokana na ufisadi huo, Rais aliivunja Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Awadhi Massawe na kusimamisha maofisa kadhaa wa bandari hiyo na wengine wanaohusika na usimamizi wa bandari kavu.

Aidha, alimsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Rished Bade na maofisa wengine wa mamlaka hiyo, ambao miongoni mwao tayari wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kutokana na ubadhirifu huo.

Kutokana na hilo, Rais Kagame kupitia kwa Balozi wake nchini, Uegene Kayihura, amempongeza Rais Magufuli kwa hatua alizochukua kusafisha uozo katika bandari hiyo, ambayo Rwanda inapitisha asilimia 70 ya mizigo yake. Dk Magufuli jana alikutana na kufanya mazungumzo na Balozi Kayihura Ikulu jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo hayo, Balozi Kayihura aliwasilisha salamu za pongezi kutoka kwa Rais Kagame ambaye alimpongeza Dk Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Tanzania.
Kwa mujibu wa Balozi Kayihura, Rais Kagame amefurahishwa na hatua ambazo Rais Magufuli anazichukua hasa katika usimamizi na utendaji kazi wa bandari na kumhakikishia kuwa Rwanda iko tayari kushirikiana na Tanzania hasa kuitumia Bandari ya Dar es salaam ambayo hupitisha asilimia zaidi ya 70 ya mizigo ya Rwanda.
Aliongeza kuwa Rwanda na Tanzania ni nchi marafiki na majirani, hivyo kuna kila sababu ya kujenga ushirikiano madhubuti katika sekta ya uchumi. Rais Magufuli alimuomba Balozi Kayihura, kumfikishia Rais Kagame salamu za shukrani kwa kumpongeza kuchaguliwa kuwa rais wa Tanzania na kwamba amedhamiria kuimarisha zaidi ushirikiano na Rwanda.

Alimhakikishia Balozi Kayihura kuwa Serikali yake ya Awamu ya Tano, itaendelea kushirikiana na Rwanda ili wananchi wa nchi zote mbili wanufaike kimaendeleo. Katika hatua nyingine, Dk Magufuli amemhakikishia Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Dk Tonia Kandiero kuwa Serikali yake itaendelea kushirikiana na benki hiyo katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Dk Magufuli alisema hayo jana Ikulu jijini Dar es Salaam, alipokutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi huyo. Pamoja na kumhakikishia ushirikiano, Rais Magufuli alitoa mwito kwa benki hiyo kupunguza michakato ya kuelekea katika utekelezaji wa miradi na badala yake ameshauri uwepo utaratibu wa haraka unaowezesha kuanza kwa miradi katika kipindi kifupi baada ya fedha kutolewa.

Kwa upande wake, Dk Kandiero pamoja na kumpongeza Rais Magufuli kwa kuchaguliwa kwake kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Awamu ya Tano, amemhakikishia kuwa benki iko tayari kuendelea kushirikiana na Tanzania katika maendeleo kama ambavyo imekuwa ikifanya na kwamba kwa sasa imetenga dola bilioni 2.3 kwa ajili ya kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo.

Alisema katika mipango yake, ADB imelenga kujielekeza katika utoaji wa mikopo katika sekta ya nishati na usafiri. Naye Dk Magufuli aliipongeza ADB kwa kuamua kujielekeza katika sekta hizo za nishati na usafiri na pia aliisisitiza kuangalia namna itakavyounga mkono mradi wa ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha kisasa.

No comments:

Post a Comment