| Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu |
TAMKO la Serikali kuhusu matangazo ya Tiba Asili na Tiba Mbadala, limesisitizwa kwamba liko palepale kwa kuwa lengo ni kuboresha huduma hiyo.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema hayo alipokuwa anazungumzia juu ya kuhusu hilo juzi jijini Dar es Salaam.
Katika tamko lililotolewa Desemba 24, mwaka huu Serikali imepiga marufuku matangazo yote yanayohusu tiba asili na tiba mbadala kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii. Kwa mujibu wa tamko hilo, wenye vibali wametakiwa kuviwasilisha pamoja na matangazo yao kwenye Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala, ili vifanyiwe mapitio.
Tamko hilo limefafanua kuwa utoaji wa elimu ya afya kwa umma unaofanywa na watoa huduma za tiba asili na tiba mbadala kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, umepigwa marufuku hadi hapo utaratibu mwingine utakapotangazwa.
Limefafanua kuwa, Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala, limeagizwa katika kipindi cha siku 14 kuanzia Desemba 24, 2015, lipitie nyaraka zote zitakazowasilishwa kuhusu usajili wa watoa huduma, usajili wa vituo vyao pamoja na maduka ya dawa za asili na dawa za tiba mbadala.
Baraza hilo pia limetakiwa kupitia upya usajili wa dawa zote zinazotumika katika huduma hizo na mashine zote zinazotumika katika huduma za tiba asili na tiba mbadala.
“Mimi niko tayari kuzungumza na mtoa huduma ambaye amekwazika na tangazo hili, ili aeleze ni sababu zipi zinazomfanya asisajiliwe. Tunafanya hivi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu,” alisisitiza.
Waziri huyo alitaja idadi ya watoa huduma hiyo kuwa ni 75,000 kwa nchi nzima na kusisitiza kuwa tamko hilo ni kwa mujibu wa Sheria ya Tiba Asili na Tiba Mbadala Namba 23 ya Mwaka 2002.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama Vya Tiba Asili Tanzania (SHIVYATIATA), Abdulrahaman Lutenga alisema hakuna mganga yeyote aliyepinga tamko hilo la Serikali na kuongeza kuwa tamko lililotolewa hivi karibuni la kupinga agizo hilo la Serikali si halali kwa kuwa halikupitia katika shirikisho hilo.
“Hatutambui kampuni hii iliyotoa tamko la kupinga tangazo la Serikali kwani ni ya mtu binafsi yenye wanahisa 11,” alisema Lutenga.
No comments:
Post a Comment