| ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Dk Jacob Chimeledya |
ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Dk Jacob Chimeledya amewatafadhalisha viongozi wa Afrika kutong’ang’ania madaraka ili kutunza amani ambayo ni chachu kubwa ya maendeleo na ustawi wa taifa.
Aidha amesema kumekuwapo na vitendo vya kuhatarisha amani ambavyo husababishwa na viongozi waliopewa nafasi na wananchi kuendelea kung’ang’ania madaraka. “Hata kama muda wao umeisha na wengine wakidiriki hata kubadilisha katiba za nchi zao ili waendelea kuwa watawala na kujinufaisha nafsi zao na familia zao,” alisema.
Askofu Chimeledya alisema hayo alipokuwa akihubiri Kanisa Kuu la Watakatifu Wote la Vinghawe mjini Mpwapwa.
Askofu Chimeledya alisema kukithiri kwa vitendo vya uvunjaji wa Katiba kumesababisha uvunjifu wa amani katika nchi nyingi za Afrika na kusababisha mauaji na vifo kwa wananchi wasio na hatia. Aliwataka viongozi wa Umoja wa Afrika kuongeza nguvu katika kutatua migogoro ya nchi zote zenye machafuko ya kisiasa ili kuokoa maisha ya wana Afrika wanyonge .
Alisema hayo huku akitolea mfano wa mataifa ya Kongo na Burundi. Alisema kuwa viongozi wa nchi hizo lazima kuheshimu mifumo na Katiba za nchi zao ili kuweza kuilinda amani ya Afrika na za nchi zao na maisha ya wananchi wanaowaongoza.
Pia Askofu Chimeledya alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais mstafu wa Awamu ya Nne Jakaya Kikwete kwa kuachia madaraka katika hali ya amani na utulivu tofauti na nchi nyingi za Afrika.
Tena aliwataka Watanzania kumuombea Rais wa Awamu ya Tano Dk John Magufuli ili aweze kutekeleza majukumu yake vizuri yakiwamo ya kushughulikia changamoto zilizokuwa zikiikumba nchi yetu ikiwemo rushwa, uzembe, na kutokuwajibika.
Aliitaka jamii kila mmoja aitafute amani yake na ya mwenzake kwa kuheshimiana na kuthaminiana kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
No comments:
Post a Comment