Monday, 16 November 2015

OLE MEDEYE ATAJWA USPIKA UKAWA

 Image result for ole medeye

 Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia.
Wakati mchakato wa kumpata mwakilishi atakayewakilisha vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) katika kinyang’anyiro cha nafasi ya Uspika ukiendelea, imebainika kuwa Goodluck Ole Medeye (pichani), ndiye atakayesimama katika nafasi hiyo.

 Ole Medeye, Mbunge wa Arumeru Magharibi kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na aliwahi pia kuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi katika utawala wa awamu ya nne wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), imeelezwa ndiye atakayewania nafasi hiyo.
 Ukawa inaundwa na Chadema, Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na NLD.

 Akizungumza kuhusu swala hilo, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari, alisema hadi jana, mgombea pekee aliyekuwa anamfahamu ameshatangaza nia ya kuwania nafasi hiyo, alikuwa ni Ole Medeye.

 Alisema Ole Medeye alishachukua fomu na kuirudisha pamojana kujitangaza kuwa atawania nafasi hiyo.

 “Mimi namfahamu mtu mmoja tu ambaye ni Ole Medeye, ambaye alinifuata na kunieleza kuwa atawania nafasi hiyo, na ameshachukua fomu. Kuhusu wengine, sifahamu ni kina nani na wako wangapi,” alisema Profesa Safari.

Naye Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia, alipoulizwa kuhusu mchakato huo, alijibu kwa ufupi “ Kesho (leo), tunakwenda mjini Dodoma.”

 Mbatia alipoulizwa zaidi aeleze idadi ya wanachama waliochukua fomu, alisema hawezi kulizungumzia jambo hilo kwa wakati huo.
 Hata hivyo aliyekuwa mgombea urais kupitia Ukawa, Edward Lowassa, alisema mchakato wa kumpata mwakilishi atayewania nafasi ya Uspika kupitia Ukawa, unaendelea kwa wakati huo.

 “Hivi sasa tunavyozungumza, kuna viongozi wengine wa Ukawa wamejifungia sehemu wakilijadili suala hilo, hivyo mchakato wa kumpata mwakilishi wa nafasi ya Uspika bado, subiri hadi baadaye utajulishwa,” alisema.

 Lowassa alisema suala la kumpata mwakilishi wa Uspika, siyo la kawaida, hivyo linahitaji umakini na utaratibu wa hali ya juu kuamua na ndiyo sababu hadi kufikia jana hakukupatika kwa jina lake.
 Kesho vikao vya Bunge vinavyotarajia kuanza mjini Dodoma kwa kumtafuta Spika wa bunge hilo huku Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Ukawa vikitarajia kuchuana kupata mwakilishi wao wa nafasi hiyo..

No comments:

Post a Comment