Monday, 22 February 2016

PAWAGA WAPATA MSAADA WENYE THAMANI YA SHILINGI MILIONI 85.88/-



Image result for majaliwa
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea misaada mbalimbali yenye thamani ya shilingi milioni 85.88/- kwa ajili ya wananchi walioathirika na mafuriko kwenye vijiji vya kata ya Mlenge, tarafa ya Pawaga,  wilaya ya Iringa vijijini mkoa wa Iringa. 
Misaada hiyo imetolewa na wadau mbalimbali kutokana na mafuriko ambayo yalibomoa nyumba 82 katika kitongoji cha Kilala, kijiji cha Kisanga na kuwaacha wananchi wake bila makazi. 
Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kasanga ambako alikwenda kukagua athari za mafuriko  na kuwapa pole wananchi hao Waziri Mkuu Majaliwa amewashukuru wadau wote waliojitolea kuwachangia watu waliopata maafa kutokana na mafuriko hayo.
Wadau waliotoa misaada hiyo ni Benki ya NMB mabati 500, mifuko ya saruji 500, kilo 820 za maharage, kilo 750 za unga wa mahindi na lita 250 za mafuta ya kupikia vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 20/-. Wengine ni Mfuko wa Pensheni wa PPF uliotoa mabati 200 na mifuko ya saruji 200  vyenye thamani ya shilingi milioni 6.6/-.
Wengine ni Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) waliotoa mabati 200 na mifuko ya saruji 160 vyenye thamani ya sh. milioni 4.5/-; Kiwanda cha kusindika nyanya cha RedGold kimetoa mifuko ya saruji 100 na mabati 50 vyenye thamani ya shilingi Milioni 3/-; mbunge wa viti maalum kwa tiketi ya CHADEMA, Bi. Susan Chogisasa na wenzake wametoa mabati 150, mifuko 23 ya saruji, kilo 100 za  maharage, kilo 50 za chumvi na nguo mbalimbali vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 1.3/-.
Madiwani wa Iringa Vijijini wametoa shilingi 380,000/-, Wabunge wa Viti Maalum kupitia CCM walitoa vifaa vya sh. Milioni 1.7/-; ofisi ya CCM Mkoa wametoa vifaa vya sh. milioni 6.1/-, Kamanda wa UVCCM Mkoa wa Iringa Salim Abri ameipatia Halmashauri ya Wilaya ya Iringa shilingi milioni 5/- ili wanunue vyakula vya waliopatwa na maafa.
Naye Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambaye pia ni mbunge wa Isimani, William Lukuvi ametoa fedha taslim shilingi milioni  20/- kati ya hizo shilingi milioni  15 zikiwa ni zake na milioni 5/- ni za Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI George Simbachawene.

No comments:

Post a Comment