Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kwa kushirikiana na Taasisi binafasi
ya Karibu Tanzania Association (KTA) kwa pamoja wamezindua programu ya
maendeleo ya soka kwa wanawake vijana ili kuhamasisha usawa wa kijinsia,
uwezeshaji kijamii na kiuchumi kwa wanawake nchini itakayofadhiliwa na
Shirika la Forum Syd kutoka nchini Sweden.
Uwekaji saini wa mkataba huo wa ushirikiano umefanywa na Katibu
Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine na Mia Mjengwa Bergdahl, Mratibu wa
Programu hiyo kutoka taasisi ya Karibu Tanzania Sweden katika ofisi za
TFF zilizopo Karume.
Programu hiyo ni ya aina yake ambayo haijapata kufanyika nchini
inalenga kujenga mfumo utakaotumiwa nchi nzima katika kutoa elimu na
mafunzo kwa soka la wanawake kwenye maeneo ya ufundi (makocha), waamuzi
(refarii), uongozi na tiba kwenye michezo.
Pia itawezesha kuendeleza vipaji kwa wachezaji wanawake vijana na
kuongeza hali ya kujitambua na kujiamini kwa walengwa. Lengo ni kuongeza
idadi ya wachezaji wenye ubora na viwango kwa soka la wanawake vijana
katika ngazi zote, hivyo kuifanya programu hii kuwa nyenzo katika
kuwawezesha wanawake.
Kwa kuanzia kozi 20 za soka la wanawake vijana kwenye Vyuo 20 vya
maendeleo ya wananchi zitaanzishwa kwenye kanda saba. Jumla ya wanawake
vijana 600 ikiwamo 30 kutoka katika kila chuo cha Maendeleo ya Wananchi
watashiriki.
Katika programu hii, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto wanashiriki kikamilifu kwa kuwezesha wanafunzi na miundo
mbinu ya vyuo vya maendeleo ya wananchi vilivyo chini ya wizara hiyo
kutumika katika kufanikisha programu hii.
Mafunzo yatatolewa sambamba na mafunzo mengine ya kawaida
yanayotolewa kwenye Vyuo Vya Maendeleo ya Wananchi, kama vile maarifa ya
jumla na mafunzo ya ufundi.
No comments:
Post a Comment