Benki
Kuu ya Tanzania (BoT), kwa kushirikiana na Mfuko wa Kuendeleza Huduma
za Kifedha Tanzania (FSDT), imezindua Mwongozo wa taifa wenye lengo la
kuongeza uelewa kuhusu elimu ya mambo ya fedha kwa wananchi.
Uelimishwaji
wa wananchi kuhusu mambo ya fedha utatekelezwa kupitia “Mwongozo wa
kwanza wa kitaifa wa elimu na ulinzi kwa mtumiaji wa huduma za fedha”
(N-FEF).
Gavana
Prof. Beno Ndulu ameuzindua rasmi mwongozo huu ambao utajikita katika
kutatua changamoto zilizobainishwa katika utafiti uliopima uelewa wa
mambo ya fedha kwa watu wazima nchini Tanzania. Utafiti huu unaitwa
“Uwezo wa Kifedha Tanzania” wa mwaka 2014.
Utafiti
huo umebainisha kuwa watanzania wengi hawana elimu na ujuzi mahususi wa
masuala ya mambo ya fedha kwa ujumla, hivyo kuwanyima fursa ya kutumia
huduma za kifedha kwa faida yao.
Katika
utafiti huo imeonyeshwa kuwa upatikanaji wa huduma za fedha umekuwa na
changamoto katika maeneo mengi huku zile zitolewazo kwa njia ya mitandao
bado hazikidhi matarajio ingawa zinawafikia wateja wengi kwa sasa.
Sambamba
na hilo kumekuwa na uhaba wa nyenzo na miundombinu ya kuhifadhi na
kufikisha taarifa za fedha kwa watumiaji wa huduma hizo kwa kuzingatia
namna sahihi ya kutoa taarifa, kuwaelimisha na kuwalinda.
Kutokana
na utafiti wa “Uwezo wa Kifedha Tanzania” wa mwaka 2014 wananchi kutoka
makundi mbalimbali katika jamii hawana ujuzi wa hesabu za kawaida ambao
ndiyo msingi mkuu katika nadharia ya masuala yahusuyo mambo ya fedha.
Elimu
msingi katika masuala ya fedha umekuwa kikwazo kwa waliowengi hasa
katika uandaaji wa bajeti, kutunza kumbukumbu ya matumizi, kupanga fedha
kwa matumizi yasiyotegemewa ama ya ziada na muhimu zaidi kutunza kiasi
kwa ajili ya matumizi ya uzeeni (baada ya kustaafu).
Inaonekana
kuwa upatikanaji wa taarifa za masuala ya fedha hutegemea zaidi vyombo
vya habari kama redio, televisheni na magazeti lakini vyombo hivi kwa
sehemu kubwa, hufikisha zaidi taarifa za biashara na masoko kuliko
ambavyo vinaelimisha jamii kuhusu matumizi na upangaji wa mapato yao.
“Haya ndiyo masuala mahususi ambayo mwongozo huu wa taifa kuhusu elimu ya huduma za fedha unalenga kushughulika nayo,” alisema Prof Ndulu.
Pamoja
na kuwepo ongezeko la upatikanaji wa huduma za kifedha, mpaka asilimia
58 mwaka 2013 kutoka kiwango cha asilimia 17 mwaka 2009, miongoni mwa
watu wazima nchini, bado mwongozo huu ni muhimu ili kuleta mfumo imara
wa sekta ya fedha na Zaidi sana ili kuleta ustawi wa maisha ya
watanzania kwa ujumla.
Prof.
Ndulu anasema kutatua changamoto za kielimu kwa ujumla na hususan elimu
ya huduma za fedha italiwezesha taifa kuwa katika mwelekeo mzuri wa
kukabiliana na umasikini na kufikia malengo ya kukuza uchumi.
“Tunapaswa
kujiuliza: ni kwa namna gani wananchi hasa wale masikini na wasiokuwa
na elimu za kifedha za wanapambana kuendeleza biashara zao katika
mazingira ya soko huria na lenye ushindani kila uchwao” alisisitiza Prof. Ndulu.
Hivyo,
mwongozo huu utahakikisha watanzania wapata elimu sahihi na ya uhakika
ya huduma za kifedha pamoja na njia anazoweza nazo kujilinda katika
ushindani huu.
Vilevile
mwongozo huu umeundwa ili kutatua changamoto za kifedha zinazohusiana
na maamuzi miongoni mwa watumiaji wa huduma hizi na kuwa jumuishi na
wenye tija kwa jamii na taifa kwa ujumla.
Mwongozo wa taifa kuhusu elimu ya huduma za fedha umeandaliwa kwa kujumisha washikadau kutoka Tanzania bara na Zanzibar.
Unabainisha
changamoto zinazohusuana na uwezo wa kifedha ambazo zinahitaji
kutatuliwa kwa uwepo wa elimu ya fedha. Pia, unatoa taratibu
wakufanikisha utekelezaji wa elimu ya fedha, na mwongozo wa kitaifa wa
kuratibu elimu ya fedha nchini.
Lengo la mwongozo wa elimu ya huduma za fedha ni kuwa na wananchi na kaya zenye uwezo kifedha nchini.
No comments:
Post a Comment