SERIKALI wilayani Moshi, mkoani Kilimanjaro imesema itasaidiana na
wanaharakati wilayani na mkoani humo kuhakikisha takwimu za watoto wenye
ulemavu zinapatikana kwa haraka ili wapate huduma zinazostahili.
Hakikisho hili limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Novatus
Makunga, wakati wa uzinduzi rasmi wa maadhimisho ya siku 16 za kupinga
ukatili wa kijinsia Kanda ya Kaskazini, uliofanyika mjini Moshi, jana.
“Inasikitisha kusikia kupitia taarifa yenu kuwa upatikanaji wa
takwimu hizi ni changamoto kwa vile wanafichwa, huku ni kuwanyanyasa
watoto wa aina hii kisaikolojia na ukatili kwa watoto,” alisema.
Alitoa rai kwa wanaharakati kupitia kamati ya maandalizi ya
maadhimisho hayo, kufanya utaratibu wa kushirikiana na Uongozi wa Shule
ya Polisi Tanzania (TPS), ili kubadilishana uzoefu na kuimarisha vita
dhidi ya ukatili wa kijinsia.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi hayo, Honoratha
Nasua, alisema moja ya changamoto wanazokutana nazo ni upatikanaji wa
takwimu za watoto wenye ulemavu ambao wanahitaji msaada mkubwa.
Hata hivyo, alisema wanaharakati wameamua kuvalia njuga suala hilo
kupitia kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ya “Funguka, mlinde mtoto
apate elimu”, kuhakikisha idadi yao inapatikana na wanapata huduma
zinastahili.
Akielezea changamoto nyingine wanazokabiliana nazo, Honoratha alisema
ni pamoja na ile ya watuhumiwa wa ukeketaji kuhamishia ukatili huo kwa
watoto wachanga. Honoratha, ambaye pia ni Meneja Programu wa Asasi
Inayopinga Ukeketaji (NAFGEM), alitoa mwito kwa wadau mbalimbali kutoa
ushirikiano wao wa dhati kutokana na ukeketaji kuwafanya waathirika
kuona wameshakuwa watu wazima na kuacha shule ili waolewe.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali
linashughulika na haki za Binadamu na jinsia la Kwieco, Elizabeth Minde,
alitoa rai kwa wazazi kujenga tabia ya kuwlainda watoto kwa saa 24, ili
kuwaepusha vitendo vya ukatili dhidi yao.

No comments:
Post a Comment